Taasisi huru isiyo ya kiserikali kutoka nchini Marekani inayoitwa ISACA tawi la Tanzania kwa kushirikiana na kampuni ya Norway inayoshughulikia maendeleo Afrika Mashariki (Norway Registers Development East Africa Limited –NRD-) wameandaa semina ya usalama wa matumizi ya kompyuta na mitandao yake katika nyanja mbalimbali kwa mashirika ya umma, benki, serikali na watu binafsi.Semina hiyo
inayotarajiwa kufanyika Agosti 28 hadi 30 mwaka huu katika Hoteli ya Nashera mkoani Morogoro ambapo Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Mhe January Makamba anatarajiwa kuwa mgeni rasmi .
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar Es Salaam Rais wa ISACA Bw. Boniface Kanemba ameeleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kutokana na ongezeka la wizi wa mitandao na matumizi mabaya ya mitandao uliojitokeza katika miaki ya hivi karibuni.
“Mafunzo haya ni kwa ajili ya wadau mbalimbali kutoka sekta zote za umma na binafsi pia kutoka nchi zote tano za Afrika Mashariki zikiwemo, Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kutokana na nchi hizi kuwa na changamoto sawa na ongezeko la wizi wa mitandao “alisema Kanemba.
Rais huyo wa ISACA ameongeza kuwa changamoto kubwa ya wizi wa mitandao inatokana na kuongezeka kwa matumizi ya mitandao ya simu katika kutuma na kupokea pesa.
Hivi karibuni, makampuni ya simu yamekuwa yakitumia mtandao mfano M-pesa na Tigo Pesa kutuma hela kwa wateja ambapo kumekuwa na kesi nyingi za wizi kwa kutumia miamala hiyo pamoja na upotevu wa nyaraka muhimu za makampuni binafsi ,umma na Serikali.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa NRD East Afrika Sebastian Marondo akizungumzia umuhimu wa semina hiyo amesema, “sio jukumu la serikali peka yake kupambana na uhalifu bali ni jukumu la kila mwananchi ,makampuni na mashirika binafsi katika kulinda na kujenga nchi yetu.”
ISACA ni taasisi huru ya kimataifa isiyokuwa ya faida inayohusika katika kusimamia na kutoa mafunzo na maarifa ya mifumo ya mitandao wakati NRD East Afrika ni kampuni inayojihusisha na mifumo ya mitandao ya kompyuta na usalama wake.