Daah! Ali manusura vijana wa Mourinho waione Wembley mwaka huu baada ya kuwafunga nyuki wa kaskazini mashariki mwa Ujerumani, Borrusia Dortmund mabao 2-0 usiku huu katika dimba la Santiago Bernabeu
Matokeo hayo yameitupa nje Real Madrid kutokana na matokeo ya mchezo wa kwanza nchini ujerumani ambapo Mourinho alipiga kipigo cha mbwa mwizi cha mabao 4-1 na baada ya kushinda leo kwa mabo mawili Madrid wanatoka kwa wastani wa mabao 4-3.
Mchezo wa leo ulikuwa mgumu sana kwa Mourinho kwani walilazimika kumaliza kipindi cha kwanza wakiwa 0-0 na kipindi cha pili kilipoanza bado mambo yalikuwa magumu mpaka dakika ya 83 ambapo waliandika bao la kwanza kupitia kwa Mfaransa Karim Benzema akipokea pasi nzuri kutoka kwa Mjerumani Mesut Ozil.
Na katika dakika ya 88 beki machachari Sergio Ramos alimalizia pasi maridhawa ya Karim Benzema na kuzamisha gozi kambani, lakini matokeo hayo hayajafua dafu kufuatia kipigo cha 4-1 ugenini.
Katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo Real Madrid walicheza vizuri zaidi ya wapinzani wao lakini walishindwa kupangua ngome imara ya Kocha Flopp aliyetamba toka awali kuwa hawataweza kuwafunga, lakini kipindi cha pili waliachia na kufungwa, kama Madrid wangekuwa makini wangewatoa leo baada ya kupoteza nafasi muhimu.
Ozil hatasaulika kwa mashabiki wa soka wa Real Madrid baada ya kupoteza nafasi muhimu za kufunga mabao ambayo yangewapeleka dimba la taifa la Wembley nchini Uingereza kucheza mchezo wa fainali.
Waswahili wana msemo wao usemao “Mwenzako akinyolewa zako tia maji”, Madrid safari yao imekwisha leo usiku huku wakiathiriwa na matokeo ya mchezo wa kwanza, watani zao wa jadi, FC Barcelona nao kesho wanapambana na Wekundu wa kusini mwa Ujerumani FC Bayern Munich katika dimba la Camp Nou huku Barca wakiwa na kumbukumbu ya kutandikwa mabao 4-0 Allianz Arena.
Je yatawafika ya Madrid leo ama watafunga mabao 5-0 ili wafuzu fainali na hatimaye kukutana na Dortmund ambao wameshakata tiketi leo usiku.


VIKOSI VYA TIMU ZOTE
Real Madrid: Diego Lopez, Essien, Varane, Sergio Ramos, Fabio Coentrao, Modric, Alonso, Di Maria, Ozil, Ronaldo, Higuain.
Subs: Casillas, Pepe, Khedira, Kaka, Benzema, Albiol, Morata.
Borussia Dortmund: Weidenfeller, Piszczek, Subotic, Hummels, Schmelzer, Gundogan, Bender, Blaszczykowski, Gotze, Reus, Lewandowski.
Subs: Langerak, Kehl, Leitner, Sahin, Grosskreutz, Schieber, Felipe Santana.
Mwamuzi: Howard Webb









