KIKAO CHA MAANDALIZI KABLA YA MAWASILISHO YA BAJETI YA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI BUNGENI CHAFANYIKA MJINI DODOMA NA TAMKO LA WAZIRI NCHIMBI JUU YA MLIPUKO WA BOMU ARUSHA





Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Emmanuel Nchimbi aliyekaa katikati akitoa maelekezo kwa Watendaji Wakuu wakiwemo Wakuu wa Idara na Maafisa Bajeti wa Taasisi zote za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika Kikao cha ndani cha maandalizi kabla ya mawasilisho ya Bajeti ya Wizara hiyo inayotarajiwa kusomwa kesho mjini Dodoma, kilichofanyika katika ofisi za Wizara hiyo mjini Dodoma.

Sehemu ya Watendaji Wakuu wa Idara na Taasisi za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakishiriki katika mapitio ya nyaraka za bajeti ya wizara hiyo katika kikao cha ndani cha Maandalizi kabla ya Mawasilisho ya Bajeti ya Wizara hiyo inayotarajiwa kusomwa kesho mjini Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Emmanuel Nchimbi aliyevaa shati jeupe akimuelekeza jambo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mbarak AbdulWakil wa pili kutoka kulia akifuatiwa na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Mwamini Malemi katika Kikao cha ndani cha maandalizi kabla ya mawasilisho ya Bajeti ya Wizara hiyo inayotarajiwa kusomwa kesho mjini Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali itachukua hatua kali kwa mtu yeyote atakayebainika kuhusika na tukio la mlipuko wa bomu lililosababisha mauaji ya mtu mmoja na kujeruhi wengine 59 wakiwemo watano waliojeruhiwa vibaya katika tukio lililotokea leo katika kanisa Katoliki Parokia ya Olasiti mjini Arusha.

Waziri Nchimbi amewataka watanzania kuwa watulivu wakati huu na kuviachia vyombo vya dola kufanya kazi yake na kwamba watanzania wanapaswa kuchukua tahadhari juu ya watu waovu wanaotaka kuwavuruga na kuwafarakanisha kwa misingi ya dini.

Akihojiwa na waandishi wa habari waliofika ofisini kwake leo mjini Dodoma Waziri Nchimbi amesema tukio hilo limetokea Mjini Arusha leo majira ya saa tano ya asubuhi wakati waumini wa Parokia hiyo walipokuwa wakiendelea na ibada ya misa kanisani hapo iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Arusha Josephat Lebulu pamoja na Balozi wa Vatican hapa nchini Fransis Padila .

Waziri Nchimbi amesema tayari Jeshi la Polisi linawashikilia watu sita kwa ajili ya mahojiano juu ya tukio hilo na kwamba tayari Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Amme Silima na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IJP) Said Mwema wako mjini Arusha kusimamia hali ya usalama mjini humo.

Amesema kwa sasa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la polisi inashirikiana na Wizara ya Ulinzi limeanza uchunguzi ili kuwabaini waliohusika na tukio hilo ikiwemo chanzo cha tukio hilo pia.

Aidha ametoa pole kwa wote waliofiwa na ndugu yao, waliojeruhiwa, Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha Josephat Lebulu pamoja na Balozi wa Vatican Nchini Tanzania Askofu Mkuu Fransis Padila” amesema Waziri Nchimbi.
Previous Post Next Post

Popular Items