GAZETI LA MTANZANIA: POMBE YA VIROBA KUPIGWA MARUFUKU





SERIKALI inakusudia kupiga marufuku pombe iliyohifadhiwa katika paketi maarufu kwa jina la kiroba, kama hatua ya kulinda afya za watumiaji.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi alitoa taarifa hiyo bungeni juzi jioni wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge wakati akihitimisha mjadala kuhusu bajeti ya wizara yake.



“Wizara yangu kwa kushirikiana na wizara ya viwanda na biashara tutafanya uchunguzi, tukijiridhisha tutapiga marufuku pombe hiyo,” alisema.

Dk. Mwinyi alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalumu, Lediana Mng’ong’o (CCM) aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kupiga marufuku pombe hiyo.

Mng’ong’o alisema pombe hiyo imekuwa na athari kubwa katika jamii hususan kundi la vijana ambao baadhi wamekuwa wakishinda vijiweni bila kujitambua.

Mbunge huyo alisema si tu pombe hiyo inaathiri afya za watumiaji, lakini pia imekuwa ikiathiri shughuli za uzalishaji mali katika jamii.

Akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara yake, Dk. Mwinyi alisema anatambua madhara kutokana na matumizi ya pombe ya viroba.

“Tutalifanyia kazi suala hilo, tunatambua kuwa pombe ina madhara makubwa kwa afya na jamii. Kijamii pombe imekuwa moja ya vyanzo vya ajali barabarani,” alisema.



Source: Gazeti la Tanzania Daima May 11,2013, mwandishi ni Khamis Mkotya, Dodoma .
Previous Post Next Post