TAREHE 23 - 24 APRILI 2013 Tarehe 23 - 24/04/2013, Mhe. Begum K. Taji, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa alifanya ziara ya kikazi Lyon, mji wa pili kwa utajiri baada ya Paris. Akiwa Lyon, Balozi Taji alihudhuria mkutano ulioandaliwa na kampuni ya Wintech Global na washirika wake.
Madhumuni ya mkutano huu ambao kauli mbiu yake ni ‘Clear Vision of the Crude Oil Market’ ni kuwafahamisha wadau wa sekta ya mafuta kuhusu kipimo maalum kinachotarajiwa kuzinduliwa na kampuni hii kwa ajili ya kupima kiwango cha tindikali kinachopatikana kwenye mafuta mazito (crude oil). Kiwango cha tindikali ndicho kinachoamua bei ya mafuta haya katika soko la dunia.
Kwa mujibu wa Wintech mpaka hivi sasa hakuna kipimo maalum kwa ajili ya kupima tindikali katika mafuta haya. Washiriki wa mkutano huu walikuwa ni wadau wa sekta hii ikiwa ni pamoja na makampuni ya mafuta, nchi zinazozalisha mafuta na zile zinazotegemea kuchimba mafuta katika siku za usoni.
Baadhi ya mabalozi kutoka nchi za Afrika hususan nchi za Afrika Mashariki walialikwa kuhudhuria mkutano huu. Pamoja na kuhudhuria mkutano huo, Mhe. Balozi Taji alipata fursa ya kukutana na watu mbalimbali kwa ajili ya kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya utalii, biashara na uwekezaji.
Baadhi ya watu aliokutana nao ni Bw. Philippe Grillot, Rais wa Chama cha wafanyabiashara na wenye viwanda wa Lyon.
Katika mazungumzo yao walikubaliana kuandaa mkakati maalum utakaofanyika Lyon kwa ajili ya kuelezea fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana Tanzania na kuyakaribisha makampuni hayo kuwekeza katika sekta za kilimo; nishati; miundombinu; utalii na madini. Vile vile, Mhe. Balozi Taji alifanya mahojiano na ‘radiopluriel’ na kutumia fursa hii pia kuitangaza Tanzania.
Mhe. Balozi Begum K. Taji akiwa na wakuu wa kampuni ya WINTECH GLOBAL ambao ni waandaaji wa mkutano huo uliofana sana.
Balozi Begum K. Taji akiwa na baadhi ya washiriki. Kulia kwa Balozi Taji ni Balozi wa Msumbiji anayewakilishia nchi yake Ufaransa.
Balozi Begum K. Taji akiwa pamoja na Bw. Juvenal Noel, mtangazaji wa Radio Pluriel. Kituo hicho ni moja ya vituo vikubwa sana nchini Ufaransa na Balozi alipata fursa nzuri kuitangaza Tanzania na vivutio vyake