WIZAYA YA MAENDELEO YA JAMII KUZINDUA WA MPANGO KAZI WA KUZUIA UKATILI DHIDI YA WATOTO KESHO

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inatarajia Kuzindua Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kuzuia Ukatili dhidi ya Watoto, utakaohusisha wadau mbalimbali wanaosimamia ustawi wa watoto nchini mpango utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu

Lengo la uzinduzi wa mpango huu ni kuandaa mazingira mazuri ya kisera, sheria, mikakati na miongozo kuhusu upatikanaji wa haki za watoto hapa nchini ikiwemo kuzuia vitendo vya ukatili dhidi yao, mpango utakaotekelezwa kati ya mwaka 2013 hadi 2016.

Uzinduzi wa mpango huu unatarajiwa kufunguliwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Mhe. Jenista Mhagama (Mb), utakaofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Dodoma, mkoani Dodoma siku ya Ijumaa ya tarehe 12 Aprili 2013, saa 7:00 mchana.

Uzinduzi wa mpango huo utakwenda sanjari na semina ya siku mbili itakayowashirikisha wadau mbalimbali wa idara za ustawi wa watoto nchini ikiwamo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto; Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii; Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi; Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, TACAIDS, UNICEF, asisi zisizo za kiserikali na za dini.

Mpango kazi huu umeandaliwa mahususi kufuatia kuwapo kwa matukio megi ya kikatili yanayowakuta watoto ikiwamo vitendo vya kutupa na kutelekeza watoto, kubakwa na kulawiti, kukata viungo vya watoto wenye ulemavu wa ngozi, watoto kuchwa moto sehemu za miili yao, vitendo vinavyoashiria mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Utafiti wa kina wa hali ya ukatili wa watoto hapa nchini wa mwaka 2009-2011 umebainisha kukithiri kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto ambapo watoto wa kike 3 kati ya 10 na mvulana 1 kati ya 7 wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Ongezeko hili kubwa la unyanyasaji wa watoto kwa siku za hivi karibuni lilipelekea Serikali kuandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 na kutunga Sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009 kwa lengo la kuendeleza, kuboresha, kuhifadhi na kulinda haki za mtoto.

Wizara inatoa wito kwa wananchi na watendaji wote hasa katika ngazi za mkoa, wilaya, kata na vijijini na mtaa kutoa ushirikiano wa kutosha katika kuutekeleza mpango kazi huu ili kuhakikisha kuwa watoto wanalelewa na kuishi kwa amani, upendo na usalama.

E. T. Ching’oro

Kny: KATIBU MKUU

10/04/2013
Previous Post Next Post