Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ibrahimu Kilongo akionyesha bastola iliyokutwa toka kwa watuhumiwa watatu waliokamatwa kwenye moja ya nyumba ya kulala wageni iliyopo eneo la Sombetini jijini Arusha.Mbali na bastola hiyo pia watuhumiwa hao walikutwa na risasi 41 za silaha hiyo.
___:Arusha:__
Jeshi la polisi mkoani hapa limefanikiwa kuwatia mbaroni majambazi watatu wakiwa na bastola aina ya browning yenye no.016080 pamoja na risasi zake 41 huko maeneo ya Shamsi kata ya Elerai jijini hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kaimu kamanda wa polisi mkoani hapa kamishna msaidizi wa polisi Ibrahim Kilongo alisema kuwa huko maeneo ya shamsi kwenye bar ya Tarakea walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa na bastola hiyo iliyokuwa na risasi 13 kwenye magazine na baada ya kwenda kuwapekuwa kwenye nyumba ya wageni ya Honolulu waliwakuta na risasi zingine 28
Kilongo aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kwenye tukio hilo kuwa ni Hashimu Abdallah 59 mkazi wa KIhonda mkoani morogoro na mwingine ni Omari Husein Ludanga 40 mkazi wa Morogoro na mwingine ni Gibson Ngosi 56 mkazi wa Gairo.
Kaimu Kamanda alisema kutokana na upelelezi uliofanyika matukio mawili tofauti waliwabaini watuhumuwa hao wakishirikiana na mwenzao Raphael Robert walishiriki kwenye matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha kwenye matukio mawili yaliofanyika tarehe tofauti 13,16 ya mwezi wa 3 mwaka huu jijini hapa.
Alisema kuwa mtuhumiwa Raphael yeye alikamatwa pekee yake akiwa na simu iliyoibiwa kwenye tukio la kwanza maeneo ya Kijenge majira ya saa 1:30 usiku baada ya kumpiga risasi ya paja Vicky Maglan 50 na kumpora kiasi cha tsh.700,000 na simu ya mkononi akiwa anatokea dukani kwake maeneo hayo ya kijenge.
Aidha katika tukio lengine Kilongo alisema kuwa watuhumiwa hao walishiriki katika tukio la kuiba kwenye shule ya Notre Dame iliopo kwenye eneo la Njiro na kumpiga risasi Sister Mary Shobana 79 mkazi wa Njiro na kasha kunyang’anya fedha taslimu kiasi cha tsh.30 milioni ambazo alitoka kuchukuwa kwenye Benki ya Exim tawi la shoprite.
Kaimu kamanda alisema baada ya mahojiano watuhumiwa walikiri kushiriki katika matukio hayo na kuwa jeshi hili linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine walioshirikiana nao kwenye matukio hayo huku watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara upelelezi wa awali kukamilika.