Baada ya kufuzu raundi ya tatu ya kombe la shirikisho na kupangiwa timu ya jeshi la Morroco FAR Rabat, mabingwa mara mbili wa taji la mapinduzi na makamu bingwa wa kombe la Kagame, klabu ya Azam fc yenye makazi yake Mbade Chamazi nje kidpgo ya jiji la Dar es salaam, sasa imehamishia majeshi yake katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya Africa Lyon keshokutwa uwanja wa chamazi.
Akizungumza kwa kujiamini, afisa habari wa klabu hiyo, Jafar Idd Maganga amesema kamwe hawadharau mchezo wowote na ndio maana wanaendelea kujifua ili kuwakabili Lyon wanaopambana kufa na kupona kukwepa panga la kurejea ligi daraja la kwanza.
“Africa Lyon wapo makini na hawajashuka daraja, bado wapo kwenye ushindani mkubwa, tunalitambua hilo na ndio maana tunaandaa kikosi cha kwanza kwa ajili ya mchezo huo muhimu kwetu, tukipata pointi tatu zitatusaidia kupata nafasi nzuri katika msimamo na kuwakilisha taifa kimataifa mwakani”. Alisema Idd.
Afisa habari huyo aliongeza kuwa mpaka sasa wachezaji wote ni wazima, hivyo wataingia kwa nguvu zote kuwakabili wapinzani wao katika dimba la nyumbani, Chamazi Complex maaneo ya Mbande.
Akizungumzia hali halisi ya ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu, Idd alisema ushindani ni mkubwa na ndio maana kila unapoingia uwanjani, unatakiwa kutumia akili nyingi kupata matokeo ya ushindi.
“Kabla ya kuvaana na Barrack YC, tulicheza mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ruvu Shooting na kuwafunga 1-0 katika uwanja wao, tulikabiliana na changamoto kubwa kutokana na ubora wao, lakini keshokutwa tunahitaji sana pointi tatu na lazima zipatikane kulingana na uwezo wetu kwa sasa”. Alijigamba Idd.
Wakati Azam fc wakijipanga vilivyo kuwaadhibu Lyon, nao kwa upande wao wamesema maandalizi yanakwenda vizuri na wanahitaji ushindi katika mchezo huo.
Mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo, Mkenya, Charles Otieno alisema wanang`ang`a kusalia ligi kuu msimu huu na ushindi waliopata mechi mbili zilizopita umewapa nguvu kubwa, hivyo Azam lazima wajipange kweli kweli.
“Tatizo la klabu yetu ni safu ya ushambuliaji, tunapata nafasi nyingi lakini huwa tunashindwa kuzitumia, lakini kwa sasa tumefanya mazoezi ya kufunga na tunaamini siku hiyo tutafanya vizuri mbele ya wapinzani wetu”. Alisema Otieno.
Azam fc wataingia uwanjani wakiwa na ndoto za kutwaa ubingwa msimu huu wakiwa na pointi 43 nyuma ya vinara Yanga wenye pointi 49.
Afrika Lyon wapo nafasi ya 12 wakiwa na mzigo wa poniti 19 wakipambana kwa nguvu zote kusalia michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara.