WAJELAJELA WAPIGA HESABU KALI KUWAMALIZA JKT RUVU MEI MOSI CHAMAZI DAR ES SALAAM!!

Maafande wa jeshi la magereza, Tanzania Prisons “wajelajela” wapo kambini kujiandaa na mchezo wa mei mosi dhidi ya wanapiga kwata wenzao wa JKT Ruvu wanaohaha kutafuta njia ya kubakia ligi kuu msimu huu. Mtanange huo utapigwa uwanja wa Chamazi Mbande nje kidogo ya jiji la Dar es salaam majira ya saa 10 kamili jioni.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka jijini Mbeya, katibu mkuu wa klabu hiyo Sadick Jumbe alisema wao wanajifua vilivyo huku wakichagizwa na ushindi wa mechi mbili mfulululizo katika dimba la nyumbani la kumbukumbu ya Hayati Edward Moringe Sokoine jijini humo.

“Mwalimu Jumanne Chale anaendelea kunoa makali ya vijnana wetu, tunajua wenzetu JKT Ruvu wapo katika hali mbaya na wana mechi ngumu kesho dhidi ya Yanga, wiki ijayo wanacheza na Lyon na baada ya hapo watakutana na sisi Chamazi, hakika wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kwani mechi zote ni ngumu sana na sisi tuko barabara sana”. Alisema Sadick Jumbe.

Jumbe alisema kikosi kizima kipo sawa, vijana wana morali kubwa kujiandaa na mchezo huo ambapo aprili 28 wataanza safari ya kuelekea Dar es salaam tayari kwa matanange huo dhidi ya maafande wa Ruvu JKT ambao mpaka sasa hawana kocha mkuu baada ya kocha wake Charles Kilinda kubwaga manyanga kuinoa klabu hiyo.

“Nilisema toka awali kwamba mtu akifikisha pointi 26 angalau anakuwa katika hali nzuri, sisi tuna uhakika wa kubakia ligi kuu msimu huu, kila mechi kwetu muhimu sana na Ruvu JKT watambue kuwa wanakutana na wanaume wenzao ambao wako kamili kila idara kusaka ushindi”. Alijigamba Jumbe.

Katibu huyo aliongeza kuwa kamati ya saidia Prisons ibaki ligi kuu chini ya kamanda wa polisi mkoani humo, Diwani Athman Msuya akishirikiana na viongozi wa serikali pamoja na wadau wa soka imeleta hamasa kubwa na mshikamano katika kikosi chao kwani wachezaji wanajisikia furaha sana kushangiliwa na umati mkubwa wa watu.

“Hakika sasa wana Mbeya wameamua kutusaidia kwa hali na mali na ndio maana siku za karibuni timu imekuwa na ari kubwa katika mechi zilizopita, moto huu tutauendeleza mwanzo mwisho ili kupata ushindi na kujiweka nafasi nzuri zaidi”.

Katika mechi mbili zilizopita, Prisons iliwatungua bao 1-0 Mgambo JKT na ikashusha kipigo cha mabo 2-0 kwa vijana wa Charles Boniface Mkwasa, klabu ya Ruvu Shooting kutoka mabatini Mlandizi mkoani Pwani.

Endapo Prisons itafanikiwa kubakia ligi kuu msimu huu, msimu ujao wa ligi kuu Tanzania bara mkoa huo utakuwa na timu mbili zinazowakilisha wapenda mchezo wa soka jijini humo, klabu hizo zitakuwa Mbeya City chini ya kocha Juma Mwambusi na Prisons chini ya Jumane Chale.
Previous Post Next Post

Popular Items