OLJORO KUWACHINJA YANGA JUMATANO, YANGA YAJIBU MAPIGO!

images
Maafande wa Jeshi la kujenga taifa, JKT Oljoro kutoka jijini Arusha wanaendelea kupanga silaha za kuwaangamiza vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara, vijana wa mitaa ya Jangwani, Dar Young Africans, katika mchezo wa ligi kuu utakaopigwa uwanja wa taifa jumatano aprili 10.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka jijini Arusha, Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Riziki Shawa, amesema kuwa, wanajua ugumu wa wapinzani wao , lakini wanaandaa mashine za uhakika ili kuwaadhibi wakiwa mbele ya umati mkubwa wa mashabiki wao.
“Yanga inasifiwa kwa kuwa na nyota wa kimataifa, lakini mwaka huu kinachowabeba ni bahati tu, mwaka ni wao na ndio maana wanaweza kupata ushindi hata kama hawajacheza kandanda, sisi tutapambana nao kufa na kupona ili kupata ushindi”. Alijigamba Kocha Shawa.
Kocha huyo anayeonekana kujiamni zaidi  aliongeza kuwa msimu huu Oljoro kushuka daraja ni sawa na ndoto za mchana, wamejipanga kushinda mechi zilizosalia wakianza na mechi ya jumatano.
Wakati huo huo wenyeji wa Oljoro siku ya jumatano, klabu ya Yanga, inaendelea na mazoezi ya mchezo huo jijini Dar es salaam huku wachezaji wote wakiwa salama.
Akizungumza leo hii, afisa habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, amesema wanajiandaa kupata ushindi muhimu mbele ya Oljoro na kuimarisha zaidi harakati zao za kutwaa taji la ligi kuu msimu huu.
“Sisi tunaendelea vizuri na tuna uhakika wa kufika siku hiyo salama, kikubwa wana Yanga wote tushikamane wakati huu muhimu wa kulitwaa taji linaloshikiliwa na watani wetu Simba, muhimu kwa kila shabiki wetu ni kufika uwanja wa taifa jumatano”. Alisema Kizuguto.
Yanga wapo nafasi ya kwanza ya msimamo wa ligi kuu wakiwa na pointi 49 kibindoni, wakati wapinzani wao JKT Oljoro wapo nafasi ya nane wakijikusanyia  pointi 28.
Previous Post Next Post