Kufanikiwa na kuwa na ushawishi katika maisha ya kawaida ya binadamu si jambo rahisi. Mtu mwenye ushawishi ni nani?
Ni mtu yeyote ambaye vitendo vyake, kauli zake ama ushauri wake hupokelewa kwa haraka na kufuatwa na watu. Katika orodha utakayoenda kuisoma, kuna majina ambayo mara nyingi yamekuwa yakionekana zaidi kwenye habari mbaya na scandal za hapa na pale lakini namna matendo yao yanavyopokelewa na kuwa gumzo kwenye maeneo mbalimbali, yanawafanya kuwa watu wenye ushawishi mkubwa japokuwa wengine wameshindwa kutumia nafasi hiyo kushawishi masuala chanya na yenye tija kwa jamii.
Wakati mwingine si kitu rahisi kupima ushawishi lakini tutaangalia ni wazo mawazo gani ya mtu, mifano gani ya mtu, kipaji gani cha mtu na ugunduzi gani wa mtu uliobadilisha jambo katika nchi yetu. Hawa ndio mastaa 20 wa burudani, michezo na urembo Tanzania wenye ushawishi mkubwa zaidi
1. Wema Sepetu
Well, well, well kunaweza kukawa na mjadala mrefu sana hapa wa kwanini mrembo huyu akamate nafasi ya kwanza wakati kila kukicha amekuwa akigonga vichwa vya habari kwa scandals kibao. Hiyo ni kweli lakini ukiugeuza umaarufu huo wa Wema na kuupeleka katika muktadha wa biashara na jinsi anavyokubalika, hakuna anayemfikia Wema. Wema ni brand inayouzika kirahisi. Kuandikwa mara kwa mara kwenye magazeti ya udaku ambapo mara nyingi si kwa kupenda yeye, kumemfanya Wema awe dhahabu inayotamaniwa kushikwa na kila mtu. Habari za Wema hapa Bongo5 zimekuwa zikipata hits (kusomwa zaidi) kuliko habari yoyote ya staa yoyote yule unayemjua hapa Tanzania.
Iwe picha akiwa kwa daktari akingolewa jino, picha za mtindo mpya wa nywele, tattoo aliyojichora, picha za mbwa wake, Gucci na Vanny, picha zinamuonesha akiwa na shoga zake Kajala na wengine, kila kitu kuhusu Wema kinavutia attention ya watu. Story za Wema husomwa zaidi na kupata comments nyingi kuliko za wengine wote.
Kama leo hii Wema akisema aanzishe bidhaa yoyote inayowalenga vijana, haitachukua muda kushika na kutafutwa kama njugu. Wema ni show stopper! Kama akiingia ukumbini kwenye shughuli, shughuli hiyo husimama kwa muda kutokana na watu kugeuka kutaka kumwangalia kwa uzuri zaidi wakati akielekea sehemu ya kukaa. Kutoka kuwa Miss Tanzania na sasa akiwa muigizaji wa orodha A Tanzania, CEO wa kampuni ya filamu, Endless Fame Films, Wema Sepetu ni mwanamke mwenye ushawishi mkubwa.
2. Diamond
Ni msanii gani Tanzania ambaye nyimbo zake zinahit mtaani bila hata kupigwa redioni? Bila shaka umeshasikia nyimbo nyingi za Diamond mtaani siku za hivi karibuni ukiwemo UKIMWONA na ukajiuliza iweje unahit wakati haujaachiwa rasmi? Muziki wa Diamond umekuwa ukitumika kama tulizo la wanyonge walio kwenye mahaba mazito. Kuanzia Mbagala, Nitarejea, Lala Salama, Mawazo ama Nataka Kulewa, zote zimekuwa zikitumiwa na watu wa rika mbalimbali, madaraja tofauti ya kiuchumi, wanawake kwa wanaume na watoto kama burudisho la roho zao. Diamond Platnumz hi hitmaker na haoneshi dalili za kupunguza kasi.
Diamond ndiye msanii anayefanya show nyingi zaidi ndani na nje ya Tanzania na kwa kulipwa gharama kubwa kuliko msanii mwingine yeyote muda huu. Hujaza kumbi kubwa za starehe yeye mwenyewe bila backup ya msanii mwingine na kuwaacha wasichana wakibubujikwa na machozi ya furaha na kutamani walau kukishika tu kifua chake kilichoanza kupasuka kwa mazoezi.
Kwa mujibu wa kampuni ya Push Mobile, Diamond ambaye jina lake halisi ni Nasib ndiye msanii anayeuza zaidi nyimbo zake kama miito ya simu (RBT).
Pamoja na kuzungukwa na scandal kibao kuhusu wanawake, Diamond ni kijana mwenye mawazo pevu na ya kiutuuzima. Akiwa ametoka kwenye familia duni na kupata misukosuko mingi ikiwemo kutengwa na baba yake na kulelewa zaidi na mama yake, Diamond amekuwa akitoa ushauri na kuwapa moyo watafutaji wa maisha wasikate tamaa. Hupenda kutoa ushauri kwa vijana wenzie kuhusiana na umuhimu wa kujituma, kuchapa kazi, kumuabudu mwenyezi Mungu na kutokata tamaa.
Katika kuhakikisha kuwa anaitolea pia jamii, hivi karibuni alitangaza kuwa na nia ya kujenga msikiti. Ni kwa sababu zipi kijana huyu asiwe na ushawishi?
3. Millard Ayo
Japo si kituo chake cha kwanza kuanza kazi, jina la Millard lilianza kufahamika nchini kupitia kipindi cha Milazo 101 cha Radio One. Sauti yake yenye mamlaka na ubunifu hewani, ulikifanya kipindi hicho kuwa maarufu kuliko vingine vya burudani katika radio hiyo inayomilikiwa na kampuni ya IPP.
Kuondoka kwake Radio One kulikuwa ni pigo kubwa lakini lenye neema kwa Clouds FM. Alihamia Clouds FM na kuanzisha kipindi kipya kiitwacho Amplifanya ambacho kilichukua nafasi ya kipindi cha nyimbo za kiafrika, Bambataa. Haikuchukua muda kipindi cha Amplifanya kikawa miongoni mwa vipindi bora kabisa Clouds FM.
Leo hii Millard ni miongoni mwa watangazaji bora Tanzania na wanaosikilizwa zaidi. Si maarufu tu redioni bali pia ndiye mtangazaji wa Tanzania mwenye mashabiki wengi zaidi kwenye mitandao ya kijamii. Ana zaidi ya followers 40,000 kwenye Twitter huku Facebook akiwa na likes zaidi ya 90,000.
Umaarufu wake kwenye mitandao ya kijamii umemfanya ageuke brand na kuyavutia makampuni makubwa kama CRDB Bank, Fast Jet na mengine kudhamini kile anachotweet. Tweets zake tu zinamuingizia fedha huku akimiliki pia website yake binafsi yenye wasomaji lukuki. Pamoja na kupata mafanikio hayo, Millard ameendelea kuwa mchapakazi, simple, mtu anayejituma kutafuta habari hata sehemu za mbali kabisa, mcheshi na mtu wa watu.
4. Nancy Sumari
Nancy Sumari ni msichana mrembo, mpole na mcheshi. Ndiye Miss Tanzania wa kwanza aliyewahi kufika mbali zaidi kwenye shindano la Miss World ambapo mwaka 2005 alifanikiwa kuwa Miss World Africa.
Kwa sasa Nancy ambaye ni mama wa mtoto mmoja wa kike, ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anasoma Shahada ya Biashara. Pia ni mjasiriamali na anafanya kazi zake na jamii zikiwemo kuwahamasisha watoto wa kike kujitambua na kuthubutu, ili kutimiza ndoto zao.
Katika harakati zake za kuhakikisha wasichana wa Tanzania wanatambua haki zao, anaendesha programu iitwayo Mentorship, ambayo inazunguka kwenye shule mbalimbali za serikali za wasichana nchini, na kuzungumza nao kuhusu maisha. Kwenye programu hiyo, tunabadilishana mawazo na wanafunzi na wao wanazungumza changamoto wanazokutana nazo na kupeana mawazo jinsi ya kufanya kwani nawaambia wakiamua kuthubutu wanaweza kufanikiwa, na wanaonesha wanaweza,Nancy aliliambia gazeti la Habari Leo hivi karibuni.
Pamoja na hayo pia Nancy anashirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), kwenye kampeni ya kujenga mabweni ya wasichana kwenye shule za sekondari za serikali nchini, ili kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu.
Hivi karibuni alizindua kitabu chake kwaajili ya watoto Nyota Yako kinachomlenga mtoto wa kike kuona jinsi wanawake wengine walivyofanikiwa licha ya kupitia changamoto mbalimbali.
Ninaamini kitabu kitasomwa na wengi ndio maana nikaamua ujumbe wangu niufikishe kwa njia hii, watasoma watoto wetu hata wajukuu kitajenga kitu kwenye akili ya mtoto na wakisoma shuhuda za hao waliofanikiwa nao watathubutu aliliambia Habari Leo. Tanzania itegemee mengi makubwa kutoka kwa mrembo huyu.
5. Ambwene Yesaya aka AY
Safari ya AY mpaka kuja kuwa nyota anayefahamika Afrika nzima na sehemu zingine duniani haikuwa rahisi. Amepitia mengi. Aliwahi kusema kuwa kabla ya kufahamika Afrika Mashariki, alikuwa akienda Kampala na Nairobi kufanya show za bure ili tu kukuza jina lake, jitihada ambazo zilizaa matunda.
AY ni msanii smart, mbunifu, risk taker na anayeijua biashara ya muziki.
Ni msanii wa Tanzania anayefanya video za ghali zaidi ambapo mpaka sasa video zake tatu, Speak With Your Body aliowashirikisha wamarekani Lamyia Good na Romeo, Partyzone na Money zilimgharimu zaidi ya dola 70,000 kwa pamoja kuzikamilisha. Video zake zimekuwa zikichezwa kwenye vituo vikubwa vya runinga duniani.
Mwaka jana alifanikiwa kuandika historia kwa kushinda tuzo za Channel O katika kipengele cha video bora ya mwaka ya Afrika Mashariki kwa wimbo wake I dont Wanna Be Alone aliowashirikisha Sauti Sol wa Kenya. Umaarufu na busara zake ziliivutia kampuni ya simu ya Airtel mwaka jana na kumteua kuwa balozi wake. Kwa sasa ni mwenyekiti mtendaji wa kampuni ya burudani, Unity Entertainment, anajihusisha na biashara za nguo, mwanzilishi wa kipindi cha televisheni cha Mkasi na biashara zingine.
Akiwa na followers zaidi ya 40,000 kwenye Twitter, mwaka huu AY amekuwa msanii wa kwanza wa Tanzania kupata alama ya tick ya blue ya verification kwenye mtandao huo. Ni watu watano tu nchini wana alama hiyo.
6. Hasheem Thabeet
Hasheem Thabeet ni mtanzania wa kwanza kucheza kwenye ligi ya mpira wa kikapu wa kulipwa nchini Marekani, NBA. Akiwa na urefu wa 7 ft 3 Hasheem ndiye mchezaji mrefu zaidi kwenye ligi hiyo. Anacheza timu ya Oklahoma City Thunder kwa mshahara wa dola milioni 5.128 kwa mwaka.
Pamoja na kuwa Marekani muda mwingi, Hasheem hasahau ya nyumbani na hupenda sana kuongelea wasanii wa Bongo Flava kama alivyoandika.
Mwaka 2000 mpaka mwaka 2005 Juma Nature alikuwemo katika kila nyimbo ambayo ilikuwa hit ndani ya bongo. kubali au kataa. #fact.
Akitumia Twitter, Hasheem anajulikana kwa jinsi anavyopenda kuandika ujumbe wa matumaini. Hizi ni tweets 5 zenye ujumbe utiao matumaini alizoandika hivi karibuni.
No matter what u go thru in life there is no need of gettin angry with god and reflect bitterness to people around u. #havefaith.
The wise ones speak b’se they have something to say… fools speaks b’se they have to say somethin. thik before u speak. #liveandlearn.
Everything can change in a blink of an eye… but dont worry; god never blinks. #believe #havefaith
Life aint about how hard u can hit… it’s about how hard u can get hit and still move forward.
Envy is a waste of time… accept what you already have, not what u need.
7. Flaviana Matata
Flavy ni mwanamitindo wa kimataifa aliyehamishia makazi yake nchini Marekani. Amefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika fani hiyo kwa kushiriki kwenye fashion show kubwa dunia, kufanya matangazo ya brand kubwa pamoja na kuhusishwa kwenye majarida ya kimataifa.
Hivi karibuni Matata alishiriki katika kampeni za matangazo makubwa ya makampuni ya nguo ya DIESELna EDUN.
Kampeni ya DIESEL + EDUN ilianzishwa mwaka jana mwezi wa kwanza ambapo muanzilishi wa kampuni ya DIESEL – Renzo Rosso – na waanzalishi wa kampuni ya EDUN – Ali Hewson na Bono walisafiri hadi nchi za Uganda na Mali na kukutana na wakulima wa pamba barani Africa.
Waliingia makubaliano ya kutengeneza nguo maalum zitakazotokana na pamba ya wakulima hawa wa Afrika na hivyo kuwanufaisha moja kwa moja. Hivyo basi nguo hizi zinatangazwa kama kampeni ili kunufaisha bara la Afrika.
Nguo hizo zitaanza kupatikana mwanzoni mwa mwezi wa tatu katika maduka mbalimbali nchini Marekani na duniani. Pia nguo za DIESEL + EDUN zitauzwa kupitia mitandao mbalimbali.
Flaviana ambaye aliwahi kuwa Miss Universe Tanzania 2007 anabaki kuwa mwanamitindo pekee kutoka bara la Africa katika kushiriki katika kampeni za nguo hizo.
Alianzisha taasisi ya Flaviana Matata Foundation inayohusika kuwasaidia wasichana kupata karo ya shule, sare na mahitaji mengine muhimu. Pia hutoa mafunzo na misaada kwa wanawake ili waanzishe miradi mbalimbali ili kujiongezea kipato.
8. Loveness Diva
Diva Love Loveness ni mtangazaji maarufu zaidi wa vipindi vya usiku. Ujasiri wake wa kuzungumza masuala ya mapenzi bila kificho umemtengenezea maisha ya pande mbili, kupendwa sana na kuchukukiwa sana. Ana mashabiki wengi.
Mara kadhaa kauli zake zimewahi kuleta mijadala mizito nchini lakini bado kipindi chake cha Ala za Roho cha Clouds FM kimeendelea kuwa kipindi chenye wasikilizaji wengi zaidi ukilinganisha na vipindi vingine vya aina hiyo katika vituo mbalimbali vya radio nchini.
Diva pia hujihusisha na shughuli za kusaidia wasiojiweza kupitia mradi wake wa Diva Giving for Charity.
9. Masanja Mkandamizaji
Huenda watu wengi wanaweza wakawa hawafahamu kwamba Masanja ndiye staa wa Tanzania mwenye likes nyingi Facebook, 104,670 na zaidi. Masanja ni miongoni mwa wachekeshaji wa kizazi kipya wenye mashabiki wengi zaidi. Umaarufu wake umetokana na kipindi cha Ze Komedi kilichoanzisha EATV na sasa kikiwa TBC 1. Pamoja na kuwa mchekeshaji, Masanja ni muimbaji wa nyimbo za injili, mchungaji mtarajiwa na mambo mengine. Huzitumia akaunti zake za mitandao ya kijamii kuchekesha na kuwafurahisha zaidi followers wake na ni miongini mwa mastaa wanaopata comments nyingi zaidi kila wawekapo status.
10. Fid Q
Fareed Kubanda si rapper anayeheshimika tu kama mwandishi mkali wa mashairi, bali pia anatambulika kwa kujihusisha kwake na shughuli za kijamii.
January mwaka huu, Taasisi ya Under The Same Sun inayojihusisha na kutetea haki ya watu wenye ulemavu wa ngozi, albino nchini, ilimtunuku cheti cha shukrani kwa mchango wake katika kampeni ya shirika hilo.
Alipata cheti hicho baada ya mwaka jana kujumuika na taasisi hiyo katika ziara yao ya kanda ya ziwa akiwa kama muelimishaji kwenye vita dhidi ya mauaji ya ALBINO.
Kujituma kwenye uchapaji kazi na utaratibu wa kuwa na nidhamu kazini ni moja kati ya vitu vilivyowafurahisha, aliiambia Bongo5.
Pia mwaka jana Fid alikuwa akiendesha darasa la hip hop la hiari jijini Dar es Salaam.
Akielezea madhumuni yake, Fid alisema, Kwa haraka haraka hip hop darasa maudhui yake ni kuwafundisha vijana wawe na positive thinking na attitude kwa jamii, yaani wawe na fikira zilizopo katika mstari ulio sahihi na hata kitabia, kwahiyo tunawajenga hivyo kupitia muziki wa hiphop.
11. Lady Jaydee
Mpaka sasa Lady Jaydee ana albam tano na hivi mwezi ujao ataachia albam ya sita aliyoipa jina NOTHING BUT THE TRUTH. Ndiye msanii wa kike Tanzania anayeheshimika na mwenye mafanikio zaidi. Jaydee ni mjasiriamali ambaye hutumia pia kipato anachokipata kwenye biashara zake kusaidia watu wanaohitaji msaada hususan watoto yatima wanaolelewa kwenye vituo maalum.
Mwaka huu Lady Jaydee ambaye ana likes zaidi ya 47,000 Facebook na followers zaidi ya 22,000 Twitter, aliweka historia kwa kufanikisha safari ya kuupanda mlima Kilimanjaro na kuwa msanii wa kwanza wa kike nchini kufanya hivyo.
12. Jacob Stephen
Jacob maarufu kama JB, ni muigizaji ambaye wachambuzi wa filamu za Tanzania wanadai kuwa msanii pekee wa kiume anayeweza kufikia mafanikio ya marehemu Steven Kanumba. Ni muigizaji wa kiume anayependwa zaidi kwa sasa na filamu zake zimekuwa kivutio kwa watu wengi wa kila rika. Ana uzoefu wa zaidi ya miaka 14 kwenye sanaa ya uigizaji.
Kwa sasa anamiliki kampuni ya filamu iitwayo Jerusalem ambayo imesaidia kuwaibua wasanii wengine akiwemo Rose Ndauka, Elizabeth Kiyumba Nikita na wengine.Pamoja na kuwa muigizaji pia JB ni mhubiri wa masuala ya dini.
13. Jokate Mwegelo
Jokate ni mtangazaji wa TV (Channel 0), muigizaji wa filamu, mwanamuziki na mjasiriamali. Umaarufu wake ulianza aliposhiriki shidano la Miss Tanzania mwaka 2006 na kukamata nafasi ya pili na kupata ubalozi wa Redd’s na gazeti la The Citizen.
Jokate amewahi pia kushinda tuzo za ZIFF kama muigizaji bora wa kike. Pamoja na hivyo hujihusisha na muziki pia ambapo amewahi kushirikishwa na AY kwenye wimbo Kings and Queens na hivi karibuni amesikika kwenye wimbo wa Lucci, Water up.
Hivi karibuni alijiingiza kwenye biashara ya ubunifu wa mitindo kwa kuanzisha kampuni na brand ya Kidoti ambayo hubuni nguo pamoja na kutengeneza nywele za aina mbambali zinazopatikana nchini.
14. Rita Paulsen
Maadam Rita anafahamika zaidi Facebook kwa wafuasi wake zaidi ya 25,000 kama mwanamke mwenye ushauri muhimu kuhusu maisha. Ni mwanzilishi wa shindano kubwa la kusaka vipaji vya kuimba nchini, Bongo Star Search ambalo limefanikiwa kutoa vipaji vingi na kwa kuwazawadia washindi vitita vya pesa. Ni mcheshi, mrembo na ambaye siku zote hupenda kuwapa moyo hata wale ambao uwezo wao ni mdogo.
15. Profesa Jay
Profesa Jay ni miongoni mwa wasanii waliyoifanya Bongo Flava ipate mafanikio. Akiwa na albam nne mpaka sasa, Machozi Jasho na Damu 2001, Mapinduzi Halisi 2003, J.O.S.E.P.H 2006 na Aluta Continua 2007, Prof amewahi kushinda zaidi ya tuzo 6 mbalimbali zikiwemo za Kili. Mpaka sasa hits zake zikiwemo Bongo Dar es Salaam, Jina Langu, Zali la Mentali, Nikusaidije na zingine zinaendelea kutoa burudani isiyo na kifani katika masikio ya mashabiki wake.