………………………………………………
Ligi kuu soka visiwani Zanzibar iliyosimama kwa wiki moja kupisha sherehe za pasaka ,inatarajiwa kuendelea kushika kasi aprili nne mwaka huu kwa viwanja mbalimbali kuwaka moto.
Akizungumza kwa njia ya simu na mtandao huu kutoka visiwani Zanzibar, katibu mkuu wa chama cha soka visiwani Zanzibar, Masud Ettei, amesema patashika la ligi hiyo limetawaliwa na ushindani mkubwa hususani kwa timu zinazowania taji na zile zinazopambana kukwepa rungu la kushuka daraja.
Katibu huyo alisema vinara KMKM wanashindana kufa na kupona na wapinzania wao wa karibu klabu ya Chuoni FC, pamoja na timu za Mafunzo na Zimamoto, ambazo kwa pamoja zinawania ubingwa msimu huu.
“Ushindani wa timu ni mkubwa sana, lakini hali ni hatari zaidi kwa timu za Malinzi, wakongwe Zanzibar, Mundu ,Super Falcon na Duma ambazo zinachuana kukwepa mkasi wa kuporomoka daraja”. Alisema Ettei.
Kuhusu timu kutumia vijana, Ettei alisema Zanzibar makinda wanacheza sana ligi ya huko, kwani kila timu ina wachezaji yosso wasiozidi miaka 24 pamoja na wakongwe wachache katika vikosi vyako.
“sisi ZFA mara nyingi tunahimiza soka la vijana, timu za ligi kuu zinaonekana kuwaamini vijana wadogo na kuwatumia zaidi, hali hii imepelekea makinda wengi kupata nafasi ya kuonesha vipaji vyao katika soka la ushindani”. Alisema Ettei.
Pia Ettei aliongeza kuwa mashabiki wa soka visiwani humo mara zote wanaikubali sana ligi ya huko licha ya kuwepo changamoto za hapa na pale ambazo ni suala la dunia nzuri.
Akizungumzia mikakati yao, katibu huyo alisema ZFA inafanya jitihada kubwa kuifanya ligi hiyo iwe na ushindani mkubwa pamoja na ubora wa kutosha ili kuvutia zaidi wawekezaji katika mchezo wa kandanda.
Pia alisema wanatambua kuwa soka la kisasa ni kutumia vijana wadogo wenye uwezo mkubwa na kasi kubwa, hivyo wanajipanga kupanua wigo zaidi kwa makinda kushiriki mashindano mbalimbali pamoja na michuano ya ligi kuu ili kupata timu bora ya Taifa.
Zanzibar ni moja kati ya wanachama wa shirikisho la soka barani Afrika CAF na timu zake huwa zinacheza ligi zake yaani kombe la shirikisho na ligi ya mabingwa barani Afrika.