Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete amekutana na Naibu Rais mteule wa Kenya Mhe William Kipchirchir Samoei arap Ruto ambaye alikuwa nchini kwa mapumziko ya Pasaka.
Akiongea na mgeni huyo katika hoteli ya Seronera iliyoko katika mbuga ya wanyama ya Serengeti mkoani Mara, Rais Kikwete amempongeza Mhe Ruto na Rais mteule wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta, kwa ushindi wao kwenye uchaguzi mkuu nchini Kenya.
Mhe Rais pia alimueleza Mhe Rutto furaha yake pamoja na kuridhishwa na jinsi uchaguzi ulivyofanyika kwa amani katika nchi hiyo.
Alielelezea matumaini yake ya kuwa urafiki uliopo kati ya Tanzania na Kenya utadumishwa pamoja na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mhe Rutto, ambaye aliwasili mkoani Mara wiki iliyopita akiwa na mke wake na watoto, ameondoka leo baada ya chakula cha mchana alichoandaliwa na mwenyeji wake.
JK akimuongoza kuelekea kwenye chakula cha mchana Naibu Rais mteule wa Kenya Mhe William Kipchirchir Samoei arap Ruto na mkewe Rachel Chebet katika hoteli ya kitalii ye Seronera katika mbuga ya wanyama ya Serengeti mkoani Mara. Mhe Ruto alikuwa nchini kwa mapumziko ya Pasaka.
JK akipozi na familia ya Naibu Rais mteule wa Kenya Mhe William Kipchirchir Samoei arap Ruto.
JK akiongea na Naibu Rais mteule wa Kenya Mhe William Kipchirchir Samoei arap Ruto
CHANZO: IKULU