Sekunde, dakika, saa zazidi kukatika kuelekea mpambano mkali wa ligi kuu soka Tanzania bara baina ya mabingwa watetezi wa ligi hiyo wekundu wa msimbazi Simba dhidi ya mabingwa mara mbili wa kombe la mapinduzi na wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Azam fc kwenye uwanja wa kisasa wa taifa jijini Dar es salaam.
Azam fc na Simba kwasasa zina upinzani mkubwa sana na kila zinapokutana hakika kipute kinakuwa kikali zaidi ya kawaida.
Simba wanaingiwa uwanjani wakiwa tayari wameshapoteza ubingwa na sasa wanahitaji hata nafasi ya pili ili kupata nafasi ya kucheza mashindano ya kimataifa mwakani wakati lambalamba wao wapo nafasi ya pili na pointi 46 wakihitaji kushinda ili kwasogelea vinara wa ligi hiyo Dar Young Africans.
Kikosi cha Azam kinaonekana kuwa imara zaidi msimu huu kutokana na matokeo wanayopata katika mechi za ligi kuu na michuano ya kombe la shirikisho, wakati Mnyama pori anahaha kweli kutengeneza kikosi kipya baada ya wachezaji wengi `Mafaza` kutemwa na kocha wake Patrick Liewig kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Mechi tatu zilizopita Simba ilicheza bila wakongwe wake, Mwinyi Kazimoto Mwitula, Amir Maftah, Ramadhan Chombo `Redondo`, Haruna Moshi Shaban `Boban`, Ferlix Mumba Sunzu, Komanbil Keita, Juma Said Nyoso na Abdallah Juma baada ya kocha Liewig kuwapiga chini.
Wachezaji Juma Kaseja, Mrisho Khalfan Ngasa `Anko`, Amri Athman Kiemba, Shomary Kapombe Jr, Masoud Nassor Cholo, walibakishwa kwenye kikosi hicho na kucheza michezo yote mitatu dhidi ya Coastal union, Kagera Sugar na Toto Africa.
Kwa sasa Kazimoto na Sunzu wamerejeshwa katika kikosi cha Simba na wanaweza kucheza katika mchezo wa leo endapo mwalimu utapiga hesabu zake vizuri.
Kwa upande wa Azam fc , wao wako kamili kado baada ya nyota wake Said Morad, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Deogratius Munish `Dida` kurejeshwa kikosini baada ya TAKUKURU kushindwa kuwakuta na hatia ya kula mlungula kama walivyoshitakiwa na klabu yao.
Mbali na nyota hao kuwepo, klabu hiyo ina wachezaji hatari katika kufumania nyavu, John Rafael Bocco, Brian Umony, Hamphrey Mieno na Kipre Herman Tchetche.
Lakini wapo wengine machachari kama Abubakar Salum `Sure Boy`, Michael Bolou, Himid Mao, David Mwantika, Khamis Mcha `Vialli` na wengineo.
Hakika mpambano huu ni mkali sana na timu zote zitahitaji ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya msimamo wa ligi kuu soka Tanzaniania bara inayoelekea ukingoni.