AJALI YA NDEGE YATOKEA JIJINI ARUSHA NA KUUA MMILIKI WA QUALITY TOURS AND TRAVELLERS



MMILIKI wa kampuni ya Quality Tours and Travellers Ltd, Joseph Sambeke maarufu kama Babu Sambeke, amefariki dunia baada ya ndege aliyokuwa akiirusha kuanguka wakati ikijiandaa kutua uwanja wa ndege wa Arusha.

Kwa mujibu wa washuhuda, tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 12:30 jioni wakati ndege hiyo aina ya MT 7 yenye namba za usajili 5H QTT ikitokea mjini Moshi.

Babu Sambeke alifariki wakati akikimbizwa kupelekwa hospitali kwa matibabu.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Ibrahim Kilongo, alithibitisha kutokea kwa ajali na kifo cha Babu Sambeke.

Kamanda Kilongo, alidai kuwa ajali ilitokea majira ya kuelekea saa moja usiku, Jumamosi na kwamba rubani wa ndege hiyo ambaye pia ni mmiliki wake alifariki wakati anapelekwa hospitali.

Alisema ndege iligonga mti kabla ya kuanguka lakini polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo.

Alisema ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria watatu haikuwa na abiria ye yote wakati akiianguka.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema wakati ndege hiyo ikijiandaa kushuka ili itue kwenye uwanja huo iligonga matawi ya miti katika eneo la Magereza hali ambayo ilisababisha kuanguka kwake.

Hata hivyo, Kamanda Kilongo, alisema uchunguzi kujua chanzo cha ajali ulitarajiwa kuanza jana alasiri baada ya kuwasili timu ya uchunguzi kutoka makao makuu ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania.

Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Arusha, Esther Dede, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Previous Post Next Post