THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898 E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com Fax: 255-22-2113425 | ![]() | PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120, DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Bharti Airtel India zimekubaliana kuanza mazungumzo rasmi ya kuiwezesha Serikali ya Tanzania kununua hisa za Airtel katika Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) katika muda wa wiki moja ijayo. Bharti Airtel India ni kampuni mama ya Airtel Tanzania Limited.
Wazo la kuanza kwa mazungumzo hayo katika wiki moja ijayo lilitolewa usiku wa kuamkia leo, Ijumaa, Machi 8, 2013, na Mwenyekiti wa Kampuni ya Bharti Airtel India, Bwana Sunil Mittal wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam.
Bharti Airtel India ni kampuni ya nne kwa ukubwa duniani miongoni mwa makampuni ya simu za mkononi.
Kampuni ya Bharti Airtel India ndiyo inamiliki shughuli za kimataifa za simu za mkononi za Airtel katika nchi mbali mbali ikiwamo Tanzania ambako kupitia Airtel Tanzania Limited inamiliki asilimia 35 za kampuni ya TTCL ambazo ilizipata wakati Airtel iliporithi hisa hizo baada ya kununua shughuli za Kampuni ya Zain Tanzania Limited. Aidha Airtel Tanzania inamiliki asilimia 60 katika Airtel Tanzania Limited.
Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Airtel Tanzania Limited zinashirikiana kwa karibu katika shughuli ya mawasiliano ya simu. Wakati Airtel Tanzania Limited inamiliki hisa katika TTCL na Airtel Tanzania Limited, Serikali ya Tanzania inamiliki 65 katika TTCL na hisa asilimia 40 katika kampuni hiyo ya Airtel Tanzania Limited.
Rais Kikwete alimwambia Bwana Mittal: “Tunafurahishwa na kazi maridadi inayofanywa na Airtel katika nchi yetu iwe katika kuwa mbia katika TTCL ama kwenye biashara ya simu za mkononi. Sisi katika Tanzania sasa tumekamilisha zoezi ya kutathmini hisa za TTCL na tuko tayari kwa mazungumzo kwa sababu tunataka TTCL ifanye kazi vizuri, tunataka kampuni hii ifanikiwe,”
Bwana Mittal alimwambia Rais Kikwete kuwa kampuni yake iko tayari katika wiki moja ijayo kuanzisha mazungumzo yanayolenga kuiwezesha Kampuni ya Airtel Tanzania Limited kuuza hisa zake kwa Serikali ambayo inaendelea kumiliki asilimia 65 za kampuni hiyo ya TTCL.
Bwana Mittal alimwambia Rais Kikwete: “Tunakubaliana na visheni yako Mheshimiwa Rais ya kuikarabati Kampuni ya TTCL. Tuko tayari kujadiliana na Serikali yako kuhusu thamani na hisa zetu katika kampuni hiyo na kama thathmini hiyo ni ya haki hatuna sababu ya majadiliano ya muda mrefu. Wataalam wangu watarejea nchini wiki ijayo tayari kwa mazungumzo na wataalam wa Serikali yako ili tulimalize hili.”
Makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Airtel Tanzania Limited yataiwezesha Kampuni ya TTCL kurudi mikononi mwa Serikali asilimia 100 na hivyo kufungua milango ya uwekezaji mpya katika kampuni hiyo ambayo miongoni mwa mambo mengi ndiyo itakuwa inaendesha na kusimamia Mkongo wa Taifa.
Rais Kikwete amemwambia Bwana Mittal kuwa Serikali yake tayari imepokea ripoti kuhusu thamani za hisa za TTCL kazi ambayo ilifanywa na kampuni inayojitegemea ya Deloitte & Touche. Ripoti hiyo ndiyo itakuwa msingi wa majadiliano kati ya Serikali na Airtel Tanzania Limited.
Bwana Mittal aliwasili Tanzania jioni ya jana akiongozana Bwana Manoj Kohli ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Shughuli za Kimataifa za Bharti Airtel India na Bwana Yajant Khosla ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Shughuli za Kampuni ya Bharti Airtel India katika Nchi za Afrika Zinazozungumza Lugha ya Kiingereza.
Ujumbe huo ulioonana na Rais Kikwete ulijumuisha Watendaji wa Airtel Tanzania Limited ambao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Limited ambaye anamaliza muda wake wa utumishi katika Tanzania, Bwana Sam Ellangallor, Mkurungezi Mtendaji, mpya Bwana Sunil Colaso na Mkurugenzi wa Masuala ya Mawasiliano na Mahusiano Bi. Beatrice Singano.
Bwana Mittal na ujumbe wake waliondoka usiku huo huo wa jana kuelekea Morocco, Afrika Kaskazini.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
8 Machi, 2013
Tags:
Social