Tume iliyoundwa kuchunguza ajali ya helikopta iliyosababisha kifo cha aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya Profesa George Saitoti na watu wengine watano, imesema kuna uwezekano mkubwa kuwa ajali hiyo ilisababishwa na makosa ya rubani.
Hakuna mtu aliyenusurika ajali hiyo iliyotokea katika mji wa Ngong nje kidogo ya jiji la Nairobi.
Kiongozi wa tume hiyo Kalpana Rawal amesema kuwa huenda helikopta hiyo ilianguka baada ya rubani kushindwa kuidhibiti kutokana na ukosefu wa mwanga wa kutosha.
Mjumbe mwingine wa tume hiyo Peter Maranga amesema inawezekana marubani wawili wa helikopta hiyo hawakuwa na uzoefu wa kutosha kuendesha ndege katika hali mbaya ya hewa.
Aidha tume hiyo imesema imegundua hitilafu katika sekta ya mafunzo na ubora wa kiufundi katika ndege.
Hali kadhalika tume hiyo imeilaumu kampuni ya Eurocopter iliyoiunda helikopta hiyo, kwa vipuri ilivyowekewa ndege hiyo siku chache kabla ya kuuzwa kwa polisi nchini Kenya.