Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwaonyesha ng’ombe wafugaji wa Kabila la Wamasai waliomtembelea katika shamba lake la mifugo kijijini Kwake Msoga,Kata ya Chalinze,wilayani Bagamoyo jana(Jumapili).(picha na Freddy Maro).
Na Freddy Maro Msoga, Bagamoyo.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ametoa wito kwa wafugaji nchini kupima na kupanga ardhi kwaajili ya ufugaji wa bora wenye tija na kuepusha migogoro kati ya wakulima na wafugaji inayotokana na ufugaji wa kuhamahama kutafuta malisho.
Rais Kikwete alitoa rai hiyo wakati alipokuwa akizungumza na wafugaji wakabila la wamasai kutoka mkoa wa Pwani na Morogoro waliomtembelea nyumbani kwake kijijini Msoga kata ya Chalinze, wilayani Bagamoyo jana(Jumapili).
“Ni lazima mtambue kwamba ufugaji wa kuhamahama hauna tija kwakuwa watu wengi sasa wametambua thamani ya ardhi wanaipima na kuimiliki na hivyo maeneo ya kuchunga mifugo yanapungua.Huu ni wakati muafaka wa kupima ardhi na kuimiliki kwaajili ya ufugaji wa kisasa,” alisema Rais Kikwete.
Sambamba na kutenga maeneo maalumu kwaajili ya ufugaji Rais Kikwete amewahimiza wafugaji hao kuotesha majani kwaajili ya malisho ya mifugo ili kuepuka upungufu wa lishe ya wanyama wakati wa kiangazi na kuhakikisha mifugo hiyo inabakia na afya njema kwa faida ya wafugaji.
Wakizungumza awali,wafugaji hao waliiongozwa na kiongozi wao Mkuu Laiboni Tikwa Moreto walimshukuru Rais Kikwete kwa kuwajengea Shule ya Sekondari kwaajili ya Watoto wa wafugaji ambayo sasa hivi ina jumla ya wanafunzi 146.
“ Tunakushukuru sana kwa kutujengea shule ya Sekondari Moreto na watoto wetu sasa wamepata fursa ya kusoma na tuna kuomba utusaidie ili tuweze kuongeza madarasa,mabweni na maji ya kutosha ili wanafunzi waliopo waweze kusoma kwa ufanisi,”walisema katika risala yao kwa Rais Kikwete.
Akijibu Rais Kikwete aliwapongeza kwa kuitunza shule hiyo na kusema kuwa maisha ya kuhamahama kwa wafugaji yanawakosesha watoto wao fursa ya kupata elimu na kuahidi kuendelea kuisadia shule hiyo ili watoto wengi zaidi waweze kunufaika na elimu ya sekondari.
Baadaye wafugaji hao walipata fursa ya kutembelea shamba la mifugo la Rais Kikwete kijijini Msoga na kujionea ufugaji wa kisasa unaozingatia kanuni bora za kitaalamu ambapo ngo’mbe mmoja anaweza kufikia uzito wa kilo miasaba.