RAIS KIKWETE AZINDUA MAABARA YA KISASA YA MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA


Mhe. Rais akikata utepe kuizindua maabara ya kisasa ya TFDA, wengine katika picha ni Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid, Mkuuwa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadiki, Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya Huduma za Jamii, Margreth Sitta, Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es salaam, Ramadhani Madabida


Mhe. Rais akiwa ameshika Tuzo ya kutambua mchango wake katika uzinduzi huo mara baada ya kukabidhiwa na TFDA.


Rais Kikwete akihutubia wageni waalikwa na wafanyakazi wa TFDA.










Rais akiwa katika maabara ya TFDA, ambapo Mkurugenzi wa Maabara Bi. Charys Ugullum akimweleza namna maabara inafanya chunguzi mbalimbali na kutoa majibu ya maswali yaliyoulizwa.

Mhe. Rais akitazama dawa bandia ambayo ilikamatwa katika soko na baada ya kuchunguzwa na maabara ya TFDA iligundulika ndani ya kidonge kumewekwa unga wa mahindi badala ya dawa. Anayetoa maelezo ni Meneja mchunguzi wa dawa, Bw. Yonah Hebron

Mkurugenzi mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo, akitoa maelezo kuhusu TFDA kwa Mhe. Rais



Rais wa Tanzania, Dkt. Kikwete akiwa ameongozana na Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo mara baara ya kuwasili na kuelekea kuzindua maabara





Rais na ujumbe wake ukitoka maabara ya TFDA na kuelekea jukwaa kuu.




Wageni waalikwa wakifuatilia hotuba ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete.




======= ======= =====

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE AZINDUA MAABARA YA KISASA YA MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA (TFDA), TAREHE 18 MACHI, 2013


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete, amezindua Maabara ya kisasa ya TFDA ya uchunguzi wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na Vifaa tiba kwa lengo la kulinda afya ya wananchi.


Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Bw. Hiiti, Sillo, alieleza kuwa mifumo ya utendaji kazi ya TFDA ni ya kiwango cha Kimataifa cha ISO/ 9001:2008, ambapo maabara hii ya TFDA inayozinduliwa ni ya kwanza barani Afrika kutambuliwa na WHO miongoni mwa maabara za taasisi za Serikali za udhibiti wa bidhaa yaani “National Regulatory Authorities”, ambapo ni moja ya maabara 23 duniani zilizotambuliwa na WHO wakati kati ya hizo saba (7) ziko Afrika na tatu (3 ) zipo Afrika Mashariki.


Katika hotuba yake baada ya kuzindua maabara ya TFDA, Dkt. Kikwete amepongeza Maabara ya TFDA kwa hatua zote ilizozifikia ikiwa ni pamoja na kupata ithibati kwenye uchunguzi wa chakula na mikrobiologia kwa kiwango cha kimataifa cha ISO/IEC 17025 toka “Southern African Development Community Accreditation Services “ (SADCAS) na kwa kuteuliwa kwa maabara hiyo na Shirika la “International Federation for Animal Health” (IFAH) kuwa maabara rejea (reference laboratory) katika uchunguzi wa dawa za mifugo kwa nchi za Afrika Mashariki.


Dkt. Kikwete pamoja na kuipongeza Menejimenti na wafanyakazi wa TFDA kwa kufanya kazi kwa uadilifu, utaalamu, uaminifu na kujituma ambako kumepelekea kufikia hatua kubwa ya mafanikio yaliyopo, alieleza kuwa “ hii ni ziara ya kihistoria kwangu na kwa kweli haya ni mafanikio makubwa kwa Serikali na Taifa kwa ujumla, TFDA imeiletea sifa Taifa na ninawapongeza kwa kuipepeza vema bendera ya Taifa”.


Aidha, Dkt. Kikwete amewataka watumishi wa TFDA kutokubweteka na mafanikio yaliyofikiwa bali kuendeleza kasi katika udhibiti wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na Vifaa tiba nchini kwa lengo la kulinda afya ya Jamii.


Aidha, Mhe. Rais ameahidi kuijengea uwezo TFDA ili kusambaza mtandao wake katika kuimarisha udhibiti wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na Vifaa tiba kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuhakikisha afya za wananchi zinalindwa.


Kutokana na ubora wa mifumo ya utendaji, TFDA imeendelea kupokea wataalam kutoka nchi mbalimbali za Kenya, Zambia, Rwanda, Uganda, Ethiopia, Nigeria, Cameroon, Sudan Kusini, Burundi, Liberia, Msumbiji na Ghana kujifunza juu ya mifumo ya udhibiti wa ubora na usalama wa chakula, dawa, vipodozi na Vifaa tiba.


Mafanikio haya ni sehemu ya safari ya kuifikia Dira ya TFDA ambayo ni kuwa mamlaka inayoongoza barani Afrika katika udhibiti wa usalama, ubora na ufanisi wa vyakula, dawa, vipodozi na Vifaa tiba kwa wote.



Previous Post Next Post