NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI MH. STEPHEN MASELE ASEMA IPO HAJA YA KUJIFUNZA KUTOKA FINLAND


1 69aac
Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya madini, Mhe. Stephen Masele, akimuonesha Balozi wa Finland nchini,Sinikka Antila ramani ya maeneo ambapo kuna madini na uchimbaji unaendelea.

Serikali imesema inahitaji kujifunza zaidi kutoka Finland hususan katika uchimbaji wa madini ili kuwa na uchimbaji wenye tija kwa taifa.Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini, Stephen Masele alipokutana na Balozi wa Finland nchini, Sinikka Antila.Masele alisema Tanzania inahitaji kujifunza masuala ya uchimbaji madini kutoka Finland kwa kuwa mazingira ya uwekezaji ya nchini humo yanashabihiana na mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania.“Unajua kampuni kubwa zinazojishughulisha na uchimbaji madini nchini Finland siyo za hapo Finland bali ni kampuni kutoka nchi nyingine yani multi-nationals na hili pia ndilo linalofanyika hapa kwetu Tanzania” alisema.


Alisema Finland haina kampuni kubwa inayojishughulisha na uchimbaji wa madini nchini humo bali kampuni zinazochimba madini ni kampuni za nchi nyingine.

“Finland wamepiga hatua sana kwa kutumia uwekezaji wa aina hii hivyo nasi hatuna budi kujifunza kutoka kwao kwa kuwa huku kwetu pia kampuni kubwa zinazoshughulika na uchimbaji mkubwa wa madini ni za kigeni na siyo za hapa kwetu” alisisitiza.

Masele aliyataja maeneo ambayo Tanzania inabidi kujifunza kutoka Finland ambayo ni utoaji wa leseni za uchimbaji madini, uwazi katika sekta ya madini na udhibiti wa mapato yatokanayo na sekta husika.

Kwa upande wake Balozi Antila alimuhakikishia Naibu Waziri kuwa Serikali ya Finland ipo tayari kutoa mafunzo kwa Maofisa wanaoshughulikia sekta ya madini na vilevile alimueleza Naibu Waziri huyo kuwa Finland ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali hususan ya kiteknolojia.

Balozi Antila alisema Finland imepiga hatua katika suala la teknolojia na alimueleza naibu waziri huyo kuwa ni vyema kwa Serikali ya Tanzania kushirikiana na Serikali ya Finland katika nyanja za teknolojia katika kukuza uchumi wa taifa.

Alisisitiza kuwa Serikali ya Finland ipo tayari kutoa ushirikiano katika kuboresha mfumo wa utoaji leseni za uchimbaji madini kwa manufaa ya taifa. Alisema mfumo wa utoaji leseni unaotumika nchini Finland umesaidia kuleta uwazi na hivyo kupelekea kuboresha mapato yatokanayo na uwekezaji wa uchimbaji madini.

Balozi Antila aliongeza kuwa vyuo vikuu vingi nchini humo vipo tayari kushirikiana na Tanzania katika masuala ya uchimbaji madini na teknolojia na alieleza kuwa tayari ushirikiano umeanza kwa kutolea mfano chuo kikuu cha Dodoma ambacho kimenufaika na ushirikiano huo kutoka kwa wataalamu wa Finland.
Previous Post Next Post

Popular Items

Kenya katika hatari ya kupata Ebola

Picha: Soggy Doggy Aongeza Familia