JAMII YATAKIWA KUTAMBUA HAKI ZA WATOTO

DSC_1513

Mkuu wa wilaya ya Ilala Raymond Mushi (wa tatu kutoka kushoto) akiwa na wadau wa watoto wakisikiliza kwa makini maazimio yaliyofikiwa katika mafunzo hayo.
Na : Frank Geofray-Jeshi la Polisi.
 
Jamii imetakiwa kuwathamini na kuwalinda watoto kwa kutambua haki zinazomlinda mtoto  ili kupunguza na kuondoa wimbi la watoto wanaoitwa wa  mitaani hapa nchini na kujenga kizazi chenye maadili.Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na wadau wanaosimamia haki za watoto kutoka
Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam wakati wa
mafunzo ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto yaliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Plan kwa lengo la kutoa elimu kwa wadau  muhimu wanaoshughulika na haki za watoto .
 
Wadau hao walibainisha kuwa jamii ndiyo yenye jukumu la kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu na maadili na kutokuwepo mitaani kwa vile hakuna mtoto aliyezaliwa na mitaa bali familia na jamii kwa ujumla hivyo kuwepo kwao ni kushindwa kuwajibika kwa wadau mbalimbali wanaopaswa kumlinda mtoto .
 
Akifunga mafunzo hayo Mkuu wa wilaya ya Ilala, Raymond Mushi amewataka wazazi,walezi na jamii kutenga muda wa kuongea na watoto wao ili kuwajengea msingi mzuri wa maisha yao kwa kuwapa elimu juu ya kukabiliana na changamoto za maisha.
 
Alisema wazazi wengi siku hizi hawakai na kuongea na watoto wao kwa kisingizio cha majukumu ya kimaisha jambo ambalo siyo sahihi kwa kuwa watoto nao wana nafasi yao ya kusikilizwa na wazazi wao.
 
 Kwa upande wake mwakilishi wa Jeshi la Polisi wilaya ya Ilala Mrakibu wa Polisi Lucy Kakulu akitoa uzoefu wa ulinzi na usalama wa mtoto katika mafunzo hayo alisema ni vyema jamii ikalitumia dawati la jinsia na watoto kuripoti vitendo vya ukatili wa kijinsia ili kuwasaidia watoto kuweza kupata haki zao za kisheria.
 
Bi.Kakulu alisema changamoto wanayokumbana nayo katika madawati ya jinsia ni pamoja ushirikiano mdogo wanaoupata kutoka kwa baadhi ya familia na makabila ambayo yanaona ni fedheha na aibu kwa mambo yanayohusiana na ukatili wa kijinsia kupelekwa katika vyombo vya sheria na jamii kutambua uovu huo.
 
Naye Meneja wa Shirika la kimataifa la Plan ofisi ya Ilala Bw.Daniel Kalimbya ameiomba serikali kuliangalia kwa makini suala la watoto wadogo kuingia katika kumbi za starehe na sehemu za kuangalia mipira kwa kuwa kwa kiasi kikubwa linawaathiri watoto tangu wakiwa wadogo hivyo kuwaathiri maisha yao yote jambo linalopelekea kujenga kizazi kisicho na maadili.
 
Mafunzo hayo ya siku tatu yalishirikisha wadau kutoka Jeshi la Polisi, Idara ya Ustawi wa Jamii, Mahakama pamoja na asasi zisizo za Kiserikali na mada mbalimbali zilitolewa ikiwemo ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Mtoto, Sheria ya mtoto ya mwaka 2009 na usalama wetu kwanza.
Previous Post Next Post