WEZI WAMUUWA MWENYE SHAMBA ZANZIBAR



DSC03000
Kamishna wa Polisi Mussa Ali Mussa akifafanua jambo katika moja ya mikutano yake na Waandishi wa Habari 
………………………………………………………….
Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi
Mzee mmoja mkazi wa Kitopeni mkoa wa Kaskazini Unguja Zanzibar Bw. Ali Khamis Ali (65), ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni na watu wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kaskazini Unguja, ACP Ahmada Khamis, alisema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa 8.00 mchana huko kwenye eneo la Kitope mashambani.


Alisema Marehemu Mzee Ali ambaye pia ni imamu wa Msikiti wa Kitope mkoani hapo, alikuwa amekwenda shambani kwake kukagua mazao yake ikiwemo minazi.
Amesema alipofika shani hapo aliwaona vijana waliokuwa wakiangua nazi na wengine wakiwa chini ya mnazi wakiziandaa ili kuondokanazo kwa maana ya kuziiba. 
Kamanda Ahmada amesema baada ya Marehemu kuwabaini wezi hao, inaonekana kuwa alianza kupandana nao lakini walimzidi nguvu na kumchona na kitu hicho chenye ncha kali ambacho kinaaminika kuwa ni kisu.
Amesema eneo la tukio walikuta rungu na ala la kisu ninachoaminika kumuulia marehemu. Amesema eneo la tukio hilo pia kulikuwa na damu nyingi na lilikuwa  limevurugwa kutokana na mapambano.
Kamanda alisema baadhi ya wananchi wameitambua rungu hiyo kuwa ilikuwa ya marehemu aliyokuwa akiitumia kwa kulindia mazao yake ambayo mara kwa mara yamekuwa yakiibwa na wezi.
Kamanda Ahmada amesema kuwa pamoja na marehemu huyo kuuawa lakini inaonekana pia mmoja wa wezi hao wa mazao naye amejeruhiwa katika mapambano hayo kwani kulionekana michirizi na matone ya damu ya mtu aliyeondoka eneo la tukio na kutokomea kusikojulikana.
Amesema uchunguzi wa tukio hilo umeanza na amewataka wananchi kutoa taarifa Polisi endapo watawaona watu ama mtu mwenye majeraha ili akamatwe kwa kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.
Hata hivyo Kamanda Ahmada alisema kuwa mauaji hayo ni ya kuwania mali na ametaka kutohusishwa na hisia za imani yoyote ama za kisiasa, kishirikina, wivu wa kimapenzi, kulipiza kisasi ama imani za kidini.
“Haya ni mauaji ya kawaida na hayana hisia zozote. Ni mauaji kama mauaji mengine yanayotokea katika maeneo mengine ya nchi yetu.” Alisema Kamanda Ahmada na kuwaonya wananchi kutoweka hisia tofauti na tukio lenyewe.
Amewaomba pia Waandishi wa Habari kutowema maoni yao binafsi wanaporipoti taarifa za tukio hilo ili kuepuka kuwatia hofu wananchi.
Previous Post Next Post