WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameunda Tume maalum itakayofanya uchunguzi wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ambayo yalitangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa Februari 18, mwaka huu.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa Jumatatu wiki hii, asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne Oktoba, 2012 walifeli.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Peniel Lyimo amesema Tume hiyo ambayo inatarajiwa kuanza kazi wakati wowote wiki ijayo inajumuisha wadau kutoka Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tanzania Association of Managers and Owners of Non-Government Schools/Colleges (TAMONGSCO), Taasisi za Dini zinazotoa huduma ya elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Asasi zisizo za Kiserikali (NGOs) zinazoshughulikia masuala ya elimu.
Wadau wengine watatoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA).
Amesema Serikali inawaomba wadau wa elimu, wazazi, walezi na wananchi wote kwa ujumla watoe ushirikiano kwa Tume ili iweze kufanya kazi yake kwa ufanisi.