Oscar Pistorius.
Polisi nchini Afrika Kusini imemteua Luteni Jenerali Vineshkumar Moonoo kuwa mpelelezi mkuu mpya ya kesi ya mauaji inayomkabili mwanariadha wa nchi hiyo Oscar Pistorius.
Uteuzi huo umefanyika baada ya mpelelezi aliyekuwa akiongoza uchunguzi huo Hilton Botha, kufunguliwa mashtaka ya kuhusika na jaribio la mauaji.
Imethibitishwa kuwa Botha atafikishwa mahakamani mwezi Mei mwaka huu kujibu makosa saba ya kujaribu kuua.
Botha na maafisa wengine wawili wa polisi wanatuhumiwa kulifyatulia risasi gari lililokuwa limebeba abiria saba mwaka 2011.
Pistorius mwenye umri wa miaka 26, bingwa wa michezo ya Olimpiki ya walemavu, ameshtakiwa kwa mauaji, baada ya mpenzi wake mwanamitindo Reeva Steenkamp kuuawa kwa kupigwa risasi tarehe 14 mwezi huu nyumbani kwa mwanariadha huyo..
Kesi ya kusikiliza ombi lake la kupatiwa dhamana itaendelea leo.