TANESCO YABAINI UTAPELI KATIKA UUNGANISHAJI WA UMEME



SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limebaini uwepo wa mtandao wa matapeli unaowarubuni wananchi kwa kuwafungia umeme kwa gharama ya juu huku wakitumia punguzo la mwezi Januari kama nguzo ya utapeli.
Matapeli hao wamekuwa wakiwapa hofu wananchi kuwa punguzo la bei ya kuunganisha umeme katika makazi ya watu lililotolewa na shirika hilo mwezi uliopita  ni la miezi mitatu tu.
Akitoa tahadhari kwa wananchi kuhusu utapeli huo, kupitia taarifa iliyotolewa kwa  vyombo vya habari, Meneja wa Mawasiliano wa Tanesco,Badra Masoud  alisema wananchi wajihadhari na matapeli hao na wasikubali kurubuniwa iwapo watakutana nao.
Alisema watu hao hujiita madalali ambapo huwa wanawaomba fedha  wananchi kwa kuwajengea hofu juu ya upatikanaji wa huduma za Tanesco na kusisitiza kuwa watawapatia wateja hao huduma kwa haraka zaidi.
“Punguzo hili la gharama ya kuunganisha umeme halina kikomo na endelevu hivyo mtu asikubali kudanganywa kwa aina yeyote na wateja wahakikishe wanalipa malipo katika ofisi za Tanesco na si vinginevyo,” alisema Masoud.
Alisema Serikali kupitia Tanesco imepunguza gharama za umeme ambapo umeme wa njia moja (single phase) kwa wateja wadogo mijini umepungua kwa wastani wa asilimia 30 huku vijijini ukipungua kwa wastani wa asilimia 70.
Alisema kuwa kuunganishiwa umeme wa njia moja(single phase) na kwa kutumia nguzo moja itakuwa Sh337,340 kwa wteja wa vijijini na wale wa mijini watalipa Sh515,618 badala ya Sh1,351,884 zinazolipwa hivi sasa.
“Punguzo hilo ni sawa na wastani wa asilimia 75.02 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 61.86 kwa wateja waishio mijini” aliongeza Masoud.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa kwa wateja watakaounganishiwa njia moja(single phase) kwa kutumia nguzo mbili watalipa Sh454,654 kwa waishio vijijini na wakati wale wa mijini watalipa Sh696,760 badala ya Sh2,001, 422 iliyokuwa ikilipwa awali.Taarifa hiyo iliongeza kuwa punguzo hilo ni sawa na asailimia 77.28 kwa wateja waishio vijini wakati wale waishio mijini ni sawa na punguzo la asilimia 65.19 na kwamba viwango hivyo vilianza kutumika tangu mwezi uliopita.

Previous Post Next Post

Popular Items

Wajue Wanamuziki 10 Matajir Africa

Video: Flavour – Ikwokrikwo