SWAHILI FASHION WEEK KUFANYA ONYESHO LA MITINDO ZANZIBAR



Onyesho kubwa la mavazi Afrika Mashariki na kati la Swahili Fashion Week, limepanga kufanya onyesho kubwa visiwani Zanzibar katika Hoteli ya Mbweni Ruins siku ya Ijumaa ya tarehe 15/02/2013 ambapo wabunifu nguli kutoka Tanzania bara na Visiwani wamethibitisha kwa shauku na hamu kubwa ya kuacha kumbukumbu nzuri ndani ya...
usiku huo wa onyesho la mitindo katika visiwa hivyo vya marashi ya karafuu.
Tukio hili la Swahili Fashion Week Zanzibar litawaleta kwa pamoja zaidi ya wabunifu kumi kutoka ndani ya nchi kuonyesha ubunifu na umahiri wao katika tasnia ya sanaa ya ubunifu na kuongeza kasi ya maendeleo ya tasnia ya mitindo nchini Tanzania huku ikitangaza dhana nzima ya kujali vitu vinavyotengenezwa Afrika (Promote Made in Africa Concept)
“Maandalizi yameshika kasi, tuko tayari kupeleka ladha ya Swahili Fashion Week katika visiwa vya Zanzibar, Kama inavyofahamika kwamba watu wengi watakuwa visiwani humo kufuatilia Sauti za Busara, huu ni mwezi wa burudani na vitu vizuri kwa watu wote Zanzibar, timu ya Swahili Fashion Week inafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba inatibu kiu ya wapenzi wote wa Swahili Fashion Week na wadau wa maswala ya Ubunifu na Mitindo Zanzibar” Alisema Mustafa Hassanali muanzilishi na muandaaji wa Swahili Fashion Week.
“Kupeleka Swahili Fashion Week kwa mashabiki waliopo visiwani Zanzibar, ni kuendeleza utamaduni wetu wa kuwa tukio bora la burudani na biashara katika tasnia ya mitindo, tukio hili la Zanzibar litawashirikisha wabunifu nguli toka bara na visiwani kuonyesha ubunifu na ladha tofauti za kiutamaduni, na wapenzi wa ubunifu na mitindo kupata ladha kutoka kwa wabunifu wa ndani ikiwa ni kama sehemu ya kuongeza familia yetu ya mitindo na ushirikiano baina ya wabunifu wa bara na visiwani” Aliongezea Hassanali
Baadhi ya wabunifu watakaoshiriki ni Asia Idarous (Mshindi wa tuzo ya Humanitarian katika tuzo za SFW 2012), Dominick Godfrey, Subira Wahure, Ailinda Sawe, (Mshindi wa tuzo ya Origin Africa, SFW 2012), Martin Kadinda (Mbunifu Bora wa Nguo za Kiume, SFW 2012), Sarah Masenga (Mbunifu Bora Chipukizi, SFW 2011), Gabriel Mollel (Mbunifu Bora wa Mwaka na Mbunifu Mvumbuzi wa mwaka, SFW 2012), Subira Wahure, Jamila Vera Swai, Salim Ali, Ahmed Abdul pamoja na mshindi wa tuzo ya Mbunifu Anaechipukia wa SFW 2012, Lucky Creation.
“Swahili Fashion Week Zanzibar ni onyesho rasmi na la kwanza kufanyika visiwani humo, Swahili Fashion Week ilishafanya onyesho la mitindo mkoani Arusha mwaka 2011 na mipango ni kufanya maonyesho mbalimbali katika miji mikubwa hapa Tanzania” Alimalizia Meneja Uhusiano wa Swahili Fashion Week, Hassan Mrope.
Onyesho limepangwa kuanza mapema ambapo kuanzia saa moja usiku milango itakuwa wazi. Tiketi za onyesho hili zinapatikana katika Hoteli ya Mbweni Ruins na Hotspot Bistro.
Onyesho hili la Swahili Fashion Week Visiwani Zanzibar limedhaminiwa na Mbweni Ruins, ZG Tours, Daja Salon & Spa, Vayle Springs Clouds TV, Coconut Fm na 361 Degrees.
Swahili Fashion Week mpaka sasa ndio ni tukio kubwa la mitindo Afrika ya Mashariki na Kati. Ni mwaka wa sita sasa, Swahili Fashion Week ni jukwaa la wabunifu wa mitindo na vito vya urembo kutoka nchini zinazoongea Kiswahili na Bara la Afrika kwa ujumla kuonyesha vipaji vyao, kutangaza ubunifu wao na kutengeneza mtandao na wadau duniani. Dhamira kubwa ni kuweka mkazo katika ukanda huu kwamba ubunifu ni tasnia inayotengeza vyanzo vya mapato huku ikitangaza bidhaa zinazotengenezwa Afrika “Promoting Made in Africa concept”.
Previous Post Next Post