Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda akisalimiana na Sista Rosaria Gargiulo wa Shirika la Masista Waabuduo Damu ya Yesu alipowasili kwenye Kijiji cha Matumaini kinacholea watoto yatima eneo la Kisasa, Dodoma leo mchana Februari 7, 2013. Katikati ni Padre Vincent Boselli anayesimamia mradi wa kijiji hicho. (Picha na Irene Bwire – OWM)
Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda (wa pili kulia) akiwa amembeba mtoto Consolatha kwenye shule ya awali ya Kijiji cha Matumaini kinacholea watoto yatima eneo la Kisasa, Dodoma leo mchana Februari 7, 2013. Kulia ni Mwenyekiti wa UWT, wilaya ya Dodoma Mjini, Bi. Fatuma Mwenda na (kushoto) ni Mwenyekiti wa UWT Mkoa huo, Bi Salome Kiwaya. (Picha na Irene Bwire – OWM).
Baadhi ya watoto wa Kijiji cha Matumaini wakiangalia zawadi walizopelekewa leo Februari 7, 2013 na Mama Tunu Pinda wakati alipotembelea kijiji hicho. (Picha na Irene Bwire – OWM).
Neema Ntandu (wa tatu kushoto) ambaye ni mmojawapo wa watoto watatu waliokuwepo wakati Kijiji cha Matumaini kikianzishwa mwaka 2002, akimkabidhi zawadi ya sanamu ya Bikira Maria, Mama Tunu Pinda ambayo imetengenezwa na watoto wa kijiji hicho wakati Mama Pinda alipotembelea kijiji hicho leo mchana, Februari 7, 2013. (Picha na Irene Bwire – OWM).
MKE wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda ametoa zawadi mbalimbali kwa watoto zaidi ya 160 wanaoishi kwenye kijiji cha Matumaini ambacho kinalea watoto yatima eneo la Kisasa, nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Mama Pinda alizuru kijiji hicho kinacholea watoto yatima leo mchana (Alhamisi, Februari 7, 2013) akiwa amefuatana na viongozi wa Umoja wa Wanawake (UWT) mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Mwenyekiti wa UWT wa mkoa huo, Bi. Salome Kiwaya.
Akizungumza na watoto wa kituo hicho, Mama Pinda alisema ameamua kuwatembelea watoto hao ili kuwasalimia na kuwatakia heri ya mwaka mpya 2013.
Mkurugenzi wa kijiji hicho, Sista Rosalia Gargiulo wa Shirika la Masista waabuduo Damu ya Yesu alimshukuru Mama Pinda na viongozi wengine alioambatana nao kwa upendo wao na kwa kutoa muda wao kuamua kuwatembelea na kuwafariji watoto hao.
Meneja mradi wa kijiji hicho ambacho pia kinalea watoto wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, Padre Vincent Boselli, alisema kijiji hicho kilianzishwa mwaka 2002 kikiwa na watoto watatu na sasa hivi kina watoto 161 wanaolelewa kituoni hapo kwa mtindo wa familia kwenye nyumba 14 ambazo zina baba na mama wa kujitolea.
Zawadi hizo zenye thamani ya sh. milioni 1.1 ni mbuzi wawili, mchele (kg. 50), sukari (kg. 25), unga wa mahindi (kg. 50), mafuta ya kupikia (lita 40), katoni moja ya sabuni za miche, ndoo moja ya sabuni ya unga, madaftari dazeni tisa, penseli 100, vichongeo 100 na rula 100. Nyingine ni biskuti (katoni tatu), pipi (pakiti nne), juisi (katoni tisa) na khanga.