SABA WAPITISHWA KUWANIA UONGOZI TASMA


TanzaniaFootballFederation1 e8406
Release No. 023
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Februari 6, 2013
SABA WAPITISHWA KUWANIA UONGOZI TASMA
WATAALAMU saba wamepitishwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) utakaofanyika Februari 10 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA, Dk. Paul Marealle, wagombea hao wamepitishwa baada ya kufaulu katika usaili uliofanyika jana (Februari 5 mwaka huu).
Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Biyondho Ngome anatetea nafasi hiyo dhidi ya alikuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Mwanandi Mwankemwa. Nafasi ya Katibu Mkuu ina mgombea mmoja ambaye ni Nassoro Matuzya wakati nafasi ya Makamu Mwenyekiti haikupata mgombea.
Sheky Mngazija ni mgombea pekee wa nafasi ya Katibu Msaidizi kama ilivyo kwa Juma Mzimbiri aliyepitishwa kuwania nafasi ya Mhazini. Naye Hemed Mziray ni mgombea pekee wa nafasi ya ujumbe wa Kamati Kuu ya TASMA.
Nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemvutia Joakim Mshanga pekee.
Wapiga kura ni wajumbe sita wa Kamati ya Utendaji na wawakilishi watatu watatu kutoka mikoa ya Geita, Ilala, Iringa, Kagera, Kinondoni, Mtwara, Rukwa, Ruvuma na Temeke. Hivyo jumla ya wapiga kura wote ni 33.
UCHAGUZI TAFCA SASA KUFANYIKA MACHI 16
Baada ya kukwama mara mbili, wanachama wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu (TAFCA) wamepewa fursa ya kufanya uchaguzi wa chama hicho Machi 16 mwaka huu mjini Dodoma.
Kwa mujibu wa tangazo la uchaguzi huo, fomu kwa ajili ya waombaji uongozi katika TAFCA zitaaza kutolewa kesho (Febaruari 7 mwaka huu) na mwisho wa kurudisha ni Februari 11 mwaka huu. Majina ya waombaji uongozi watakaokuwa wamepitishwa yatatangazwa Februari 12 mwaka huu.
Kipindi cha kuweka pingamizi ni kuanzia Februari 13 hadi 17 mwaka huu. Usaili kwa waombaji utafanyika Februari 19 mwaka huu wakati matokeo ya usaili yatatangazwa Februari 20 mwaka huu.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF itasikiliza rufani kama zitakuwepo kati ya Februari 20 na 22 mwaka huu, na uamuzi wa rufani hizo utatangazwa kati ya Februari 23 na 27 mwaka huu.
Ada za fomu kwa waombaji uongozi zitakuwa sh. 200,000 kwa nafasi zote isipokuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na wajumbe wa Kamati ya Utendaji. Nafasi zitakazowaniwa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mhazini, Mhazini Msaidizi, Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF na wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
Fomu kwa waombaji uongozi zinapatikana kwenye ofisi za TAFCA zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Previous Post Next Post