Mgombea urais kupitia Muungano wa Cord, Waziri Mkuu Raila Odinga
WAGOMBEA urais wanaochuana vikali Kenya, Raila Odinga wa Muungano wa Cord na Uhuru Kenyatta wa Jubilee, wameendelea kukabana koo ikiwa ni siku tano kabla ya Uchaguzi Mkuu Jumatatu ijayo.Tafiti tatu tofauti zilizodhaminiwa na Nation Media Group (NMG), ambazo matokeo yake yametoka jana, zimeonyesha kuwa wagombea hao wanatofautiana kwa asilimia zisizozidi 1.5, hali inayoonyesha kuwa lolote linaweza kutokea siku ya uchaguzi. Hata hivyo, Odinga ana nafasi zaidi katika uchaguzi wa marudio.Matokeo yote hayo yamebainisha kuwa hakutakuwa na mshindi wa moja kwa moja, kwa kuwa wote hawatafikisha nusu ya kura zinazohitajika, huku utafiti ukibainisha kuwa katika mzunguko wa pili utakaofanyika ndani ya wiki tatu tangu kufanyika kwa uchaguzi wa awali, Odinga ana nafasi kubwa ya kushinda.Matokeo ya Pollster InfotrackUtafiti wa Kampuni ya Pollster Infotrack, unaonyesha kuwa kama uchaguzi ungefanyika leo, Odinga angeongoza kwa asilimia 46, Kenyatta angefuatia akiwa na asilimia 44.6, huku mgombea wa Amani, Musalia Mudavadi akiwafuata kwa mbali baada ya kupata asilimia 4.3.Kwa mujibu wa matokeo hayo ya kura za mwisho za maoni, wote wawili, Odinga na Kenyatta wameongeza kura kwa asilimia moja kila mmoja, ikilinganishwa na matokeo ya wiki iliyopita.Kwa mujibu wa sheria za Kenya, si ruhusa kufanya wala kuchapisha kura za maoni siku tano kabla ya uchaguzi.Kulingana na matokeo ya Infotrack Poll, Odinga anatazamiwa kushinda matokeo ya mzunguko wa pili kwa asilimia 49.2 huku mwenzake akiwa na asilimia 47.2.Utafiti huo unaonyesha kuwa nusu ya wapiga kura wa Mudavadi watahamia kwa Odinga wakati Kenyatta atapata wale waliowapigia kura wagombea wengine, Martha Karua wa Narc, James Ole Kiyiapi (Restore and Build Kenya) na Peter Kenneth (Kenya National Social Congress).Kwa upande wa makundi ya wagombea, Cord inaongoza kwa kuungwa mkono ikiwa na asilimia 45.8 ikifuatiwa na Jubilee (45.6%) na Amani ya Mudavadi ikiwa na asilimia 4.4.Utafiti wa Consumer InsightMatokeo ya utafiti wa Consumer Insight yanaonyesha kuwa Odinga hivi sasa anaungwa mkono na asilimia 46.8 ya wapigakura dhidi ya mwenzake, Kenyatta aliyepata asilimia 42.9. Mashabiki wa Mudavadi wamepungua kutoka asilimia 5.4 hadi 4.2.Kampuni ya Consumer Insight imebaini kuwa iwapo uchaguzi utakwenda hadi marudio, Odinga atatangazwa mshindi kwa kufikisha asilimia 50.6 dhidi ya Kenyatta mwenye asilimia 46.3.Utafiti huo wa Consumer Insight unaonyesha kuwa umaarufu wa Cord uko asilimia 47.8 wakati ule wa Jubilee ni asilimia 44.1.Utafiti wa Strategic PollsterUtafiti wa Strategic Pollster unaonyesha kuwa Odinga ataibuka mshindi kwa kupata asilimia 45.7 dhidi ya Kenyetta mwenye 43.8. Mudavadi bado ni wa tatu akiwa na asilimia 5.7.Katika uchaguzi wa marudio, Strategic Pollster inasema Odinga ataibuka kidedea kwa asilimia 51.7 huku mwenzake Kenyetta akisimama kwenye asilimia 45.7.Tafiti hizi zimetumia sampuli ya watu 2,600 wanaowakilisha wananchi 14,337,399 waliojiandikisha kupiga kura.Wagombea urais walichuana vikali kwa mara ya pili juzi katika mdahalo, ambao ulikuwa fursa ya mwisho kupimwa na wapiga kura kabla ya uchaguzi utakaofanyika Jumatatu ijayo.Kivuitu afariki duniaWakati huohuo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Kenya (ECK), Jaji Samuel Kivuitu amefariki dunia, siku tano kabla ya Uchaguzi Mkuu.Kivuitu (74) alifariki dunia saa nne usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya MP Shah ya Nairobi alikokuwa amepelekwa kutokana na mshtuko wa moyo.Kivuitu anakumbukwa na mambo mawili makubwa na Watanzania. Matukio ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya mwaka 2007 na pia kusoma Tanzania.Alizua balaa Kenya baada ya kumtangaza katika mazingira ya kutatanisha Mwai Kibaki kama mshindi wa urais mwaka 2007 na kuzua vurugu za kikabila kutokana na mpinzani wake n Raila Odinga kuamini alipokonywa ushindi.Alikuwa mmoja wa wanafunzi wa kwanza kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1961 na kumaliza mwaka 1965, akiwa katika Kitivo cha Sheria.Familia ya marehemu Kivuitu imesema mazishi yatasubiri hadi Uchaguzi Mkuu umalizike Machi 4, mwaka huu.