Februari 24, 2013.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewataka wanachama wake na wananchi kwa ujumla, kujiepusha na itendo vinavyoashiria vurugu, kwa kuwagawa Watanzania kwa misingi ya dini zao.
Rai hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida, Mgana Msindai, kwenye sherehe za uzinduzi wa kata mpya ya Kituntu, zilizofanyika katika kijiji cha Msambu, tarafa ya Ihanja, wilaya ya Ikungi.
Alisema tabia iliyoibuka katika siku za karibuni ikiwemo mauaji ya vingozi wa dini na kugombea kuchinja wanyama, hususani ng’ombe haipaswi kuungwa mkono badala yake viongozi wote wanapaswa kukemea kwa nguvu zote, ili kuepusha taifa kuingia kwenye vurugu.
“Tunaishi kwa amani miaka mingi sana, lakini leo hii hali siyo nzuri sana kutokana na harufu ya udini …tumeingiliana na baadhi ya ndugu zetu, wakristo na wengine ni waislamu, hata vyombo vya ndani tunaviheshimu sana hasa pale unapotembelewa na mwislamu,”alisema Msindai.
Alisema, kutokana na tabia ya uchochezi inayofanywa na baadhi ya wasiolitakia mema taifa, imezidi kuhatarisha amani, misingi na umoja wa kitaifa iliyoasisiwa na hayati baba wa Taifa mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.
Aidha Mwenyekiti CCM wilaya Ikungi, Hassan Tati alimuomba mwenyekiti wa CCM mkoa Msindai kuingilia kati wilaya hiyo mpya iweze kuwa na halmashauri yake ili kurahisisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Tati, kata hiyo ni kati ya 90 zilizopandishwa hadhi na serikali kuu mwaka 2010, huku mkoa wa Singida pekee ukinufaika na mgawo wa kuwa na kata 30.