KONE AWASHAURI KULIMA MTAMA NA UWELE



kone dfb82
Singida
WANANCHI wa mkoa wa Singida wametakiwa kuachana na tabia ya kuomba omba chakula serikalini kila mwaka, badala yake wajikite zaidi kwenye kilimo cha mtama na uwele, badala ya mahindi, ili kuondokana na janga la njaa.


Rai hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa Singida, Dk. Parseko Kone, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Simbalungwala tarafa ya Kinampanda, muda mfupi baada ya kukagua ujenzi wa maabara ya shule ya sekondari Kizaga.

Alisema kuwa, tatizoa la njaa kila mwaka mkoani Singida limekuwa la kujitakia kutokana na wakulima kupuuza kilimo cha mtama na uwele kwa ajili ya chakula na alizeti, pamba na asali kwa biashara.

“Kipaumbele cha mkoa ni mtama, uwele, muhogo na mazao ya mizizi, kwa biashara ni alizeti, pamba na asali…mahindi yanahitaji mvua nyingi hadi milimita 800, lakini mvua tunayopata ni milimita hadi 600 tu, hii haitoshi kabisa kukomaza zao la mahindi,”alisema Dk. Kone.

Kutokana na hali hiyo, alisema mwananchi atakayekaidi agizo hilo kwa kulima mahindi akikosa mavuno atalazimika kupata msaada kwa aliyempatia mbegu ya mahindi na aliyelima mtama au uwele akakosa, serikali itahakikisha inampatia msaada wa chakula.

Aidha Dk. Kone aliwataka wananchi kushiriki kikamilifu uchangiaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa maabara katika shule za sekondari, ili taifa liwee kuwa na wataalamu wa kutosha siku za usoni.

Alisema baada ya kufanikisha ujenzi wa sekondari za kutosha kutoka shule mbili miaka ya themanini hadi kufikia 154 mwaka huu, wananchi wahamishie kasi hiyo kwa kujenga maabara za kutosha ili kuondoa kabisa tatizo hilo mkoani hapa.

Hata hivyo katika mkutano huo baadhi ya wananchi, Hadija Mkumbo na Obeid Mkumbo walilalamika kuwa kijiji hicho hushiriki vema kuchangia miradi, hasa ujenzi wa zahanati ya kijiji lakini hawaridhiki mapato na matumizi yanayofanywa na viongozi wao.
Previous Post Next Post