JE UMESOAM HII? MBINU MPYA ZA KUSAFIRISHA MADAWA YA KULEVYA ZAANIKWA UKO MAREKANI



Miongoni mwa vazi ambalo hutumiwa na wasafirishaji 
wa dawa za kulevya. 

WAKATI nchini Zimbabwe wanawake wakitumia pampers kukuza ukubwa wa makalio yao, nchini Marekani wamekuwa wakitengeneza pampers za cocaine, ambazo huvaliwa  na kusafirisha dawa hizo nchi mbalimbali pasipo kugundulika.
Mbinu hiyo mpya imedaiwa kuwagharimu muda mrefu waandaaji kutengeneza pampers hizo na baada ya kukamilika huvaliwa kitaalamu nje ya nguo zao za ndani na huvalia suruali au baibui tayari kwa kuanza safari.
Maofisa wa forodha kwenye Uwanja wa Ndege wa JFK wamegundua mbinu hiyo mpya mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kuwatia mbaroni wanawake wawili kutoka Bronx wakiwa wamevalia madawa hayo. Wanawake hao wamekamatwa na kilogramu 6.5 za dawa za kulevya aina ya cocaine ambazo walikuwa wamezivalia kwa mtindo wa nepi nje ya nguo zao za ndani.
Kwa mujibu wa Gazeti la Dailymail la Uingereza, wanawake hao waliokamatwa baada ya kushuka katika ndege ya  JetBlue iliyotoka Jamhuri ya Dominika huko Santo Domingo ni Priscilla Pena na Michelle Blassingale, walikamatwa wakiwa na cocaine hizo zikiwa katika mwonekano wake wa asili.
Kukamatwa kwa pea hiyo ya wanawake, kulitokana na walinzi kushangazwa na hali ya mbwa waliokuwa nao kuwafuatilia zaidi wanawake hao na kuanza kufoka ilhali walikuwa hawana mizigo, jambo lililowasukuma maofisa hao kuamua kuwakagua vilivyo.
Baada ya kuchunguza kwa makini katika mizigo yao, hawakuweza kuona madawa yoyote, lakini walipojaribu kuwavua nguo zao walikutana na idadi kubwa ya dawa za cocaine yaliyokuwa yamefungwa mithili ya pampers nyuma ya makalio yao. Baada ya kugundulika na madawa hayo haramu, wanawake hao walikamatwa na kupelekwa chini ya ulinzi.
Kwa mujibu wa Dailymail, Blassingale amewekwa rumande huku akisubiri kufikishwa mahakamani na Pena ameachiliwa kwa dhamana ya Dola 150,000 (sawa na Sh240 milioni). Mwezi Oktoba mwaka jana, jasusi wa dawa za kulevya alihukumiwa kifungo cha miaka 300 jela baada ya kugeuza ndege ya American Airlines kuwa chombo kikubwa cha kusafirishia dawa hizo.
Victor Baurne (37) aliyekuwa meneja mizigo wa ndege hiyo alikamatwa katika kituo hicho hicho cha (JFK) John F. Kennedy International Airport kwa kosa la kusafirisha dawa za thamani  zaidi ya Pauni 330 za cocaine toka mwaka 2000 mpaka mwaka 2009.
Uchawi watumika kukamilisha malengo
Baurne alidaiwa kuwa kwa kipindi chote cha miaka tisa, alikuwa akisafiri mpaka Afrika kwa ajili ya kudidimiza mwonekano wowote wa kazi yake ya kusafirisha dawa hizo.
Wakati wa kesi yake, Baurne alikuwa akisafiri mara kwa mara mpaka Afrika kwa ajili ya kudidimiza kesi yake kwa uchawi, ambapo alikutana na waganga kadhaa ambao waliweka laana juu ya waendesha mashtaka, kulingana na nyaraka za mahakama.
Bourne pia alisisitiza kuwa wachunguzi wa kesi yake walikuwa wametoa maelezo ya uongo jambo ambalo lilikataliwa na mahakama.
Hata hivyo mauzauza kadhaa yalikuwa yakionekana mahakamani hapo wakati kesi ya Bourne ikiendelea kusomwa kabla ya kupewa agizo la kifungo cha miaka 300 jela.
Kiongozi huyo wa wafanyakazi wa American Airlines, Bourne alikuwa ametengeneza mamilioni ya dola ambayo aliyatumia kuhakikisha anafanya biashara yake anavyotaka, alisema hakimu Brooklyn.
“Bourne aliitumia American Airlines kama kampuni yake ya kusafirishia mihadarati, na kulifanya shirika hilo kuwa la jinai na kupuuzwa kwa ulinzi na usalama wa abiria katika kutekeleza azma yake kubwa,” mwanasheria wa Marekani Loretta Lynch alisema katika hukumu hiyo.
Waendesha mashtaka waliweza kuendesha kesi hiyo kutokana na ushahidi uliopatikana toka kwa wafanyakazi sita wa zamani wa kampuni hiyo walioko Texas ambao walikiri usafirishaji wa mihadarati.
Mashahidi hao walielezea namna walivyoweza kumbamba mara kwa mara akivuta dawa hizo kwa siri ndani ya ndege na kuwahonga maelfu ya dola ili wanyamaze kuhusu hilo.
Njia za kusafirisha dawa za kulenya
Kwa kuhifadhi tumboni: Wasafirishaji hawa humeza kete nyingi ambazo hufungwa kwa kutumia plastiki au kondomu na kuzidhibiti hadi mwisho wa safari. Njia hii ni hatari zaidi kwani wahusika humeza hadi kete 60 na kuhatarisha maisha yao, wengine hufa kabla ya kutimiza adhma yao.
Kuweka kwenye viatu au fenicha: Hizi huwekwa kwenye soli za viatu, mabegi ya gofu au fenicha wakati wa kusafirishwa.
Kwa kutumia mbwa: Baadhi hutumia mbwa kwa kuwasafirisha na kuwabebesha madawa hayo.
Watoto wadogo: Mwaka 2008 mwanamke mmoja alikamatwa kwa kujaribu kusafirisha kwa kufunga dawa hizo na kuzificha kwenye miguu ya watoto wawili waliokuwa na umri wa miaka 11 na 13.
Kwa kutumia wadudu: Huko Netherland walibaini kusafirishwa kwa dawa za kulevya kwa kutumia wadudu 100 waliokufa zenye thamani ya Dola 11,000.
Vibao vya makaburi: Baadhi ya wasafirishaji huko Marekani wamewahi kukamatwa wakivusha dawa hizo zikiwa zimehifadhiwa kwenye tundu lililochombwa kwenye kibao cha utambulisho ambacho huwekwa kwenye kaburi.
Kwa nguo za ndani: Wanawake hutumia zaidi njia hii kwa kutengeneza pochi kwenye brazia na chupi zao, ambapo huhifadhi kiwango kikubwa cha dawa hizo.

Previous Post Next Post