WAZIRI WA MALI ASILI KAGASHEKI ATEMBELEA SAO HILL


Waziri wa mali asili na Utalii Balozi Hamisi Kagasheki akitazama ramani inayoonesha sehemu ya msitu iliyovamiwa na wananchi.
---
Utangulizi
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Khamis Kagasheki amesema kuwa Wizara yake inathamini sana mchango mkubwa unaotolewa na wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka Shamba la Miti Sao Hill na kuwa Wizara itahakikisha kuwa wananchi hao wanaendelea kufaidi matunda yanayotokana na shamba hilo ili waendelee kushiriki katika kulitunza.

 Waziri Kagasheki alisema pia kuwa sheria na busara sharti itumike katika kutatua migogoro ya uvamizi katika shamba la miti Saohill.
 Mheshimiwa Kagasheki aliyasema hayo katika nyakati tofauti alipotembelea Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa juzi Ijumaa na jana Jumamosi tarehe 26 Januari 2013 kwa nia ya kusikiliza kero zilizopo wilayani humo kuhusiana na Shamba la miti la Saohill. Akiwa huko alifanya mikutano  na uongozi wa Mkoa wa Iringa, uongozi wa Wilaya ya Mufindi, watumishi wa Shamba la miti Saohill Madiwani wa Wilaya Mufindi na Wavunaji wa Wadogo wa Miti katika shamba la Saohill.
 Katika mikutano yote alijulishwa kuwa kuna kero mbili kubwa zinazolihusisha shamba la miti Saohill. Kwanza ni mgawo wa miti ya kupasua mbao kutoka katika shamba hilo ambao ulielezwa kuwa kwa mwaka 2012/13 haukuridhisha. 
 Pili ni kero ya wananchi kukosa ardhi ya kulima na kupanda miti kwa kuwa wameongezeka, hivyo wamevamia sehemu ya Shamba la Saohill na kulima mazao ya chakula pamoja na kupanda miti yao.
 Kamati ya Mgawo
Akizungumza na watumishi wa Shamba la Miti Saohill Waziri Kagasheki alisema kuwa baada ya kusoma na kuitafakari taarifa ya ugawaji atawachukulia hatua waliohusika na mgawo wa mwaka 2012/13 hususan, Meneja wa Shamba aliyekuwepo wakati wa mgawo huo  na Msaidizi wake, pamoja na mameneja wa tarafa za shamba la Saohill. Hatua hizo zitakuwa pamoja na kuwasimamisha kazi ili wapishe uchunguzi kuhusu mgawo ulivyofanyika. Kwa sasa mamemeja hao wamehamishiwa vituo vingine.

Vibali vya Uvunaji
 Katika mkutano wa Waziri Kagasheki na wavunaji wadogo, wavunaji hao walimwambia Waziri kuwa utaratibu wa uvunaji  kwa mwaka 2012/13 ulikuwa mbovu kwa kuwa kulikuwa na kigezo cha kuwa na mashine ya kuchana mbao kwanza ndipo mwombaji afikiriwe kupewa malighafi. 
 Wavunaji walisema kuwa , ili kukidhi kigezo hicho, walinunua mashine, wengine kwa mkopo, lakini baadhi yao hawakupewa mgawo. Walilalamika pia kuwa baadhi ya wale waliopata mgawo waliamua kuuza mgawo wao kwa wenye mashine maana wao hawakuwa nazo.
 Hata hivyo,  katika katika kikao hicho, wadau wengine, kama vile chama cha kupasua mbao cha SAFIA,  walisema wanaridhika na utaratibu mpya wa mgawo uliowekwa na Wakala wa Huduna za Misitu (TFS) ambao nia yake ni kukomesha biashara ya ulanguzi katika biashara ya mbao. 
 Kuhusu ugawaji wa miti ya kupasua mbao kwa wadau, Waziri Kagasheki alikubaliana na malalamiko ya wavunaji wadogo, kuwa utaratibu uliotumika katika kugawa miti mwaka 2012/13 haukuwa mzuri na usingeweza kutenda haki maana wajumbe wa Kamati ya Ugawaji ni Meneja na wasaidizi wake. Alisema haiwezekani watu wanaohusika na kuuendeleza na kuutunza msitu huo kutenda haki wakati wa kugawa mazao. 
 Waziri Kagasheki aliahidi kuwa ataiunda upya Kamati ya mgawo wa miti ya kuvuna katika Shamba la Saohill. Aidha Waziri Kagasheki alisema kuwa atavifuta vibali ambavyo havikutolewa kihalali ili vigawiwe upya. 

Uvamizi
 Waziri Kagasheki alipata fursa ya kutembelea Kijiji cha Kibengu kujionea hali ya uvamizi wa misitu ulivyo. Katika kijiji hicho baadhi ya watu katika kitongoji cha Mgwao walivamia  msitu wakajenga makazi na sasa wameshi ndani ya hifadhi kwa muda wa miaka 30.
 Waziri Kagasheki alisema kuwa mwaka jana kamati mbili ziliundwa, moja ya Wizara na nyingine ya Kitaifa, ili kuchunguza migogoro ya mipaka ya hifadhi nchini. Taarifa za kamati hizo ambazo zilifika Saohill sasa zinachunguzwa ili mapendekezo yake yachangie katika kutoa uamuzi kuhusu uvamizi katika Shamba la Saohill na sehemu zingine za hifadhi nchini. 
Awali, akisoma taarifa ya Wilaya ya Mufindi kwa Waziri, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Evarista Kalalu alisema kuwa wanachi wa vijiji sita  vikiwemo Ihomasa  na Udumuka vimevamia eneo la misitu ya asili iliyoko Sao Hill, kama vile Mufindi Scarp, na kufanya shughuli za kilimo kwa kati ya miaka 10 hadi 40.
Vile vile, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi alisema kuwa eneo la zaidi ya Hekta 1,000 linalomilikiwa na  Samba la miti Saohill limevamiwa na watu wanaotokea vijiji vya Wamimbwale, Usokami, Kibengu, Igeleke, Mapanda na Kitasengwa vyote vya Wilaya ya Mufindi kwa muda wa kati ya miaka 25 hadi 30.

 MWISHO
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
 Simu: +255 784 468047

 Tarehe 27 Januari 2013
Previous Post Next Post

Popular Items

Wajue Wanamuziki 10 Matajir Africa

AS CANNES YAMWAGIA SIFA KAPOMBE