WAZIRI MKUU WA KENYA RAILA ODINGA AZINDUA ILANI INAYOLENGA AJIRA KWA WAKENYA WOTE

WAZIRI Mkuu wa Kenya,Raila Odinga 
WAZIRI Mkuu wa Kenya,Raila Odinga amezindua rasmi ilani yake ya uchaguzi, huku akitoa kipaumbele katika kukuza uchumi wenye manufaa kwa wote.

Katika Ilani hiyo, Odinga anayewania Urais kupitia Muungano wa Cord alisema suala la ajira ndilo agenda kuu iwapo wataingia madarakani katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Machi 4, mwaka huu.

“Suala la kazi na ajira linakuwa ndiyo agenda kuu katika ilani hii inayoweka vipaumbele katika maeneo 10 muhimu kwa ajili ya ustawi wa watu wetu,” alisema Odinga katika uzinduzi wa ilani hiyo uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano ya Kimataifa (Kenyatta International Conference Centre-KICC).

Odinga alisema watahakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa kuanzisha mifuko maalumu ya kuwawezesha wanawake na vijana pia kuwahamasisha wawekezaji kwenda kwenye maeneo ya miji mipya ikiwamo Kakamega, Garissa na Meru.

Katika Ilani hiyo, Raila alisema wataboresha sekta ya kilimo wakizingatia zaidi umuhimu wa hifadhi ya chakula na kuhakikisha mbolea za aina zote zinazalishwa nchini humo.

“Ninawaahidi pia kwamba nitahakikisha ninaendeleza kwa vitendo msimamo wa Rais Mwai Kibaki kuboresha miundombinu katika maeneo yote nchini,” alisema. Katika uzinduzi wa Ilani hiyo, Makamu wa Rais ambaye ni mgombea mwenza wa Odinga, Kalonzo Musyoka alisema kwamba Muungano wa Cord ndio pekee unaoweza kuifikisha Kenya kwenye kilele cha maendeleo.

Alisema kwamba iwapo watachaguliwa na kuunda Serikali, watafanya uamuzi mgumu wa kubadili historia kwa kuwadhibiti wachache wanaomiliki kiasi kikubwa cha ardhi huku wengi wakiwa hawana fursa ya kuwa na kipande kidogo cha ardhi.
Alisisitiza kwamba Cord itasimamia utekelezaji wa maelekezo ya Katiba katika masuala yahusuyo migogoro ya ardhi.

Kuhusu elimu, alisema watahakikisha wanatoa mafunzo kwa walimu wengi zaidi ili kupunguza uhaba unaolikabili taifa kwa sasa.

“Tutaongeza idadi kubwa ya walimu kuanzia wa chekechea, sekondari na wahadhiri katika vyuo vikuu,” alisema na kusisisitiza kwamba mkakati huo utaambatana na kuhakikisha suala la umaskini linakuwa historia kwa wengi nchini humo.

Kiongozi mwingine katika wa Muungano huo, Moses Wetangula alieleza kwamba Cord ndiyo pekee inayoweza kutimiza ndoto za wananchi wa Kenya kuelekea maendeleo, akiahidi kwamba watahakikisha wanailinda na kuitekeleza kikamilifu Katiba Mpya ya nchi hiyo.

“Tunahitaji kutoa mwelekeo mpya wa maisha bora kwa siku zijazo kwa Wakenya. Hii ni fursa ya pekee kwao. Katiba iliyoundwa kwa mapenzi ya Wakenya wote itasimamiwa na kutekelezwa kikamilifu chini ya muungano huu wa Cord,” alisema.

Aliahidi kwamba huduma za afya ya msingi zitapatikana kwa wananchi wote na kwamba Serikali itaweka mazingira mazuri kwa wafanyakazi wa afya ili kuepuka migomo.



Previous Post Next Post