LIGI KUU YA VODACOM BARA TANZANIA YANG'ARA KWA UBORA AFRIKA


LIGI Kuu ya Tanzania imeshika nafasi ya 22 kati ya ligi 30 bora za Afrika katika karne ya 21, pamoja na kukamata nafasi ya 117 kati ya ligi 130 bora za duniani.

Kwa mujibu wa mtandao wa www.iffhs.de unaojihusisha na kutoa takwimu mbalimbali za mchezo wa soka, orodha hiyo imetolewa jana na kuonyesha Ligi Kuu ya Tanzania ipo nafasi ya 22, wakati Sudan ikiongoza kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ikiwa nafasi ya 13, ikifuatiwa na Uganda (18).


Pia Ethiopia (24) na Kenya (25) wakati ligi za nchini Rwanda na Burundi zikiwa hazijafanikiwa kuingia kwenye orodha hiyo ya ligi 30 bora Afrika.

Kwa miaka 12, Ligi ya Misri imekuwa ikiongoza ligi za Afrika ikifuatiwa na Ligi ya Tunisia, kwani Ligi ya Misri bado inashika nafasi ya kwanza kwa ligi za Afrika kwenye orodha ya ligi bora kwa karne ya 21.

Ligi ya Tunisia alikotimukia mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi imefanikiwa kupunguza tofauti ya pointi na ile ya Misri kwa sababu nchi ya Misri mwaka jana ilisimamisha shughuli zote za michezo.

Kulinganisha na mwaka 2011, Ligi ya Zambia yenyewe imeporomoka kwa nafasi mbili, huku ligi za Sudan, Senegal, Mali, Libya na Tanzania zenyewe zimepiga hatua moja juu.

Upatikanaji wa ligi bora duniani unaangaliwa kwa kuangalia klabu tano za nchi husika zinazoshika nafasi ya juu katika msimamo wa ligi, jinsi zinavyoshinda mechi na kufunga mabao katika mashindano mbalimbali kwa mwaka mzima.
Viwango hivyo vinategemea na matokeo yao katika ligi za ndani, makombe ya shirikisho pamoja na mabao wanayofunga kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa, Kombe la Shirikisho na mashindano ya Fifa.

Viwango vya Afrika vimeziangalia nchi zote wanachama wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ingawa siyo ligi za nchi zote zimeingia kwenye orodha hiyo ya ligi bora za Afrika.

1. Misri
2. Tunisia
3. Morocco
4. Nigeria
5. Algeria
6. Afrika Kusini
7. Cameroon
8. Ivory Coast
9. Angola
10. Zambia
11. Ghana
12. Zimbabwe
13. Sudan
14. Senegal
15. Mali
16. Libya
17. DR Congo
18. Uganda
19. Malawi
20. Botswana
21. Burkina Faso
22. Tanzania
23. Msumbiji
24. Ethiopia
25. Kenya
26. Seychelles
27. Swaziland
28. Namibia
29. Mauritius
30. Gambia

Previous Post Next Post