MGOGORO wa gesi umeingia sura mpya, baada ya viongozi wa dini mkoani Mtwara kuungana na wananchi kupinga usafirishwaji wake kwenda Dar es Salaam, huku Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, akitoa ufafanuzi wa faida za mradi huo kwa taifa.
Mbali na ufafanuzi huo, Waziri Muhongo amemlipua Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnain Murji kwa msimamo wake wa kuungana na wananchi hao, akieleza kuwa hamwelewi kwa kuwa wabunge akiwamo yeye, walishirikishwa vilivyo kwenye mradi huo na kulipwa posho lukuki.
Viongozi wa dini waliojitosa kwenye mgogoro huo ni Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Newala, Oscar Mnung’a na Askofu Mteule wa Kanisa la KKKT, Dayosisi Mpya ya Kusini Mashariki, Mchungaji Lucas Mbedule.
Kwa nyakati tofauti, viongozi hao wamepinga mradi wa kusafirisha nishati hiyo kwenda Dar es Salaam wakieleza kuwa hawaoni ni namna gani utawanufaisha wakazi wa Mtwara.
Askofu Mnung’a alisema anapingana na uamuzi wa kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam na badala yake kuishauri Serikali ijenge mitambo ya kufua umeme mkoani Mtwara.
“Lazima wananchi wa Mtwara waamke, tumejifunza kule Songosongo, gesi imekwenda Dar es Salaam, si Kilwa wala Lindi iliyofaidika na gesi ile… gesi ibaki Mtwara, mikoa ya kusini iimarishwe,” alisema Askofu Mnung’a na kuongeza:
“Hii yote ni Tanzania, hakuna ubaya wowote ile mitambo ya kufua umeme ikawekwa Mtwara… wafikirie leo hatuombei ila watu wakilipua Kidatu (Morogoro), nchi itakuwa gizani, lazima tutawanye rasilimali zetu siyo kila kitu Dar es Salaam.”
Askofu huyo alimpongeza Murji kwa kuweka wazi msimamo wake kuhusu suala hilo na kumshangaa Mbunge wa Masasi Mariam Kasembe anayeunga mkono akisema, mbunge huyo hawakilishi maoni ya wananchi.
“Nimewaambia waumini wangu kuwa tuwe tayari kutetea rasilimali yetu…. nampongeza Murji kwa kutetea masilahi ya wananchi,” alisema Askofu Mnung’a.
Askofu Mbedule alisema hapingi gesi kwenda Dar es Salaam ila hadi pale ahadi za Serikali zitakapotimizwa kwa wananchi wa Mtwara.
“Kwenye salamu zangu za Krismasi niliwaambia waumini kuwa ni wakati wa kuidai Serikali kutimiza ahadi zake kwa wananchi… wananchi wa Mtwara waliahidiwa viwanda, hakuna kiwanda hata kimoja, gesi inaondoka... hapana sikubaliani nalo,” alisema Mchungaji Mbedule na kuongeza:
“Serikali itueleze bomba la gesi kwenda Dar es Salaam litatoa ajira ngapi kwa wananchi wa Mtwara? Hilo moja, pili bomba hilo litachochea vipi uwekezaji kwa mikoa ya kusini… kama hakuna majibu ya hayo basi mimi nazuia gesi isiende Dar es Salaam.”
Alisema Rais Jakaya Kikwete aliwaahidi neema wananchi wa Mtwara kutokana na uchimbaji wa gesi na kwamba kabla ya kufikiria kuisafirisha kwenda Dar es Salaam ni muhimu ahadi hiyo ikatekelezwa.
“Zaidi ya miaka 21, Barabara ya Mtwara - Dar es Salaam haijaisha, mikoa mingine zinajengwa barabara zenye kilomita nyingi na zinakamilika na kuiacha hii ya kusini… hata juzi nimepita hapo bado barabara ni ya vumbi,” alisema.
chanzo:http://www.mwananchi.co.tz
Tags:
News