VIONGOZI wa nchi mbalimbali za Afrika wameipongeza Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kupigania utawala bora Afrika kupitia vita ya ukombozi, kushiriki kutatua migogoro ya nchi mbalimbali na hata kukubali kupokea wakimbizi.
Pongezi hizo zilitolewa kwa Watanzania kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete mara baada ya kuwa amekamilisha kuwasilisha Ripoti ya Hali ya Utawala Bora ya Tanzania kwenye mkutano wa Marais wa Umoja wa Afrika wanaoshiriki katika Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Afrika (APRM)
Rais Michael Sata wa Zambia ndiye aliyeanza kwa kuishukuru Tanzania wakati akiwasilisha ripoti ya nchi yake katika mkutano huo wa Wakuu wa Nchi za APRM.
“Bila mchango wa nchi kama Zambia na Tanzania katika kupambana na utawala mbovu wa makaburu leo Afrika Kusini isingekuwa ilipo,” alisema.
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alisema wananchi wa nchi yake hawatausahau mchango wa Tanzania katika kuwakomboa na kuwafikisha walipo sasa. Tulisaidiwa na nchi nyingi, lakini Tanzania ilitusaidia kwa namna ya kipekee kabisa.
“Wakati ule wa ukombozi tuliahidi kupitia moja ya nyimbo za ukombozi kuwa ‘tukiwa huru, hatutakusahau kamwe.’ Nikuhakikishieni kuwa hatutawasahahu,” alisema Rais Zuma akichangia kuhusu Ripoti ya Tanzania.
Rais Zuma alisema ingawa katika Ripoti ya Tanzania kuna masuala Serikali inapaswa kuyafanyia kazi kama suala la migogoro ya ardhi na jinsi ya kuhakikisha kukua kwa uchumi kunawanufaisha wananchi, Tanzania ina mengi ya kuifunda Afrika na akaeleza utayari wa nchi yake kuja kujifunza masuala ya udhibiti wa rushwa kwa viongozi na manunuzi ya umma.
Suala la Muungano lilionekana kumgusa zaidi Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegne ambaye alisifu kuwa Muungano huo unabaki kuwa wa kipekee na unaoikumbusha Afrika juu ya azma yake ya siku nyingi ya kuunda Umoja wa Nchi za Afrika.
Kwa upande wake Rais wa Senegal Marky Sall alisema Tanzania ni nchi nzuri na ambayo amepata kuitembelea katika vivutio vyake vya kitalii kama Ngorongoro na akaenda mbali kwa kuvutiwa namna Tanzania ilivyorekebisha sheria zake za madini.
Suala la udhibiti wa vurugu za kidini alilokuwa Rais Kikwete amelizungumzia kwa kina lilimgusa Rais Dk Boni Yayi wa Benin ambaye alikiri kuwa nchi yake ina tatizo kama hilo na kwamba angekuwa tayari kujifunza jinsi Tanzania wanavyokabiliana nalo.
Kukamilika kwa uwasilishaji wa Ripoti hiyo sasa kutaipa nafasi Serikali ya Tanzania kuanza kutekeleza Mpango kazi unaoainisha jinsi ya kuondoa changamoto za utawala bora zilizobainishwa.