Rais Mohammed Mursi wa Misri ameahidi kuimarisha demokrasia nchini mwake wakati wa mkutano baina yake na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani mjini Berlin.
Rais Mursi amesema kuwa Misri itafuata utawala wa sheria na haitaendeshwa na jeshi. Mursi ametoa kauli hiyo baada ya Kansela Merkel kutoa wito kufanyika mazungumzo ya kitaifa ili kutatua mzozo wa kisiasa taifa hilo ambalo limekumbwa na misukosuko ya ghasia kwa miezi kadhaa.
Ziara ya Rais Mursi hapa Ujerumani ilikatishwa ghafla baada ya kutolewa taarifa ya kutokea kwa machafuko zaidi nchini Misri hapo jana Jumatano. Waandamanaji wawili waliuawa kwa risasi karibu na uwanja maarufu kwa maandamano wa Tahriri na kufikisha idadi ya watu waliokufa wiki hii kutokana na ghasia kufikia 50.