CHAMA Cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimeanza mchakato wa Tuzo kwa Wanamichezo Bora wa Tanzania mwaka 2012.
Kama ilivyokuwa mwaka uliopita Kamati ya Utendaji ya TASWA imeamua suala la mchakato wa kuwapata wanamichezo hao lifanywe na kamati maalum nje ya Kamati ya Utendaji ya TASWA lengo ikiwa ni kupanua wigo na kuwashirikisha wadau wengi zaidi katika jambo hili nyeti.
Jukumu la Kamati ya Utendaji ya TASWA itakuwa ni kuhangaika na mambo ya wadhamini na masuala mengine yahusuyo sherehe hizo ambazo tunataka ziwe za aina yake.
Kutokana na hali hiyo Kamati ya Utendaji ya TASWA iliyokutana wiki iliyopita iliteua kamati maalum ya watu 11 kusimamia mchakato wa kuwapata wanamichezo hao, ambapo kamati hiyo inayotarajia kuanza vikao vyake Jumatano Januari 30, 2013 itakuwa chini ya uenyekiti wa mwanachama wa TASWA, Haji Manara.
Kamati ya Utendaji imemkabidhi jukumu Manara baada ya kujiridhisha pasi na shaka uzoefu wake katika masuala ya michezo na pia uzoefu wake katika mambo mbalimbali ya kiutawala, hivyo kuwa na imani kwamba ataendesha vizuri mchakato kama walivyofanya watangulizi wake.
Wajumbe saba wa kamati hiyo wanatoka nje ya Kamati ya Utendaji ya TASWA ambao ni Jane John, Dina Ismail, Jabir Idrissa, Tulo Chambo, Abdallah Mweri na ofisa mmoja ambaye ataombwa kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT), wakati wajumbe wanne wanatoka Kamati ya Utendaji ya TASWA ambao ni Grace Hoka, Zena Chande, Alfred Lucas na Amir Mhando.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
28/01/2013.