Halmashauri ya Wilaya Ya Mbarali, Mbeya, imetoa kibali cha uchimbwaji wa visima viwili kwenye vijiji vya Iheha na Nyakazombe Kata ya Miyombweni na Madibira wilayani Mbarali. Vijiji hivi ni miongoni mwa vijiji vingi vya Wilaya hiyo vyenye uhaba mkubwa wa maji. Mradi huo wa uchimbwaji visima utakaoanza mwezi Julai mwaka huu utafadhiliwa na Taasisi ya Kihisani ya The Norwich Tanzania Association yenye makao yake mjini Norwich, Uingereza.
Mapema mwaka huu, Ujumbe wa kutoka taasisi hiyo ya Uingereza ulitembelea Mbarali na kukutana na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Adam Mgoi ( Pichani) ambaye, mbali ya kuwashukuru wahisani hao kwa kuiongezea nguvu Halmashauri hiyo katika kutatua kero ya maji kwa wananchi wa Mbarali, alimwahidi Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya Norwich , Uingereza Mama Karrima Carter ( Pichani kushoto) kuwa angelisimamia jambo hilo na kuhakikisha kuwa wataalamu wake wa maji wanafika eneo husika na kufanya utafiti wa awali kujua wapi kitaalamu visima hivyo vinaweza kuchimbwa.
Kazi hiyo imekamilika na jana Jumanne, Januari 29, Halmashauri hiyo imekabidhi rasmi kibali cha kuchimbwa visima hivyo viwili. ( Pichani kulia ni Diwani wa Kata ya Rujewa, Mama Sabir. Picha hii ilipigwa mapema mwaka huu wakati ujumbe kutoka Uingereza ulipotembelea Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali)