Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam Suleiman Kova (kushoto) akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam. Kulia ni Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni ACP Charles Kenyela.
Na.Bongo 61 Team
Jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limejipanga vema kuhakikisha kuwa kuna ilinzi wa kutosha na wa uhakika katika kipindi hiki cha kuelekea Siku Kuu za mwisho wa mwaka za Krismas na Mwaka Mpya.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam Suleiman Kova amesema lengo ni kuhakikisha wananchi wa jiji la Dar es Salaam wanasherehekea siku kuu hizi kwa amani na utulivu kwa kuwa uzoefu unaonyesha kuwa mara nyingi katika kipindi hiki watu wenye nia ovu hujiandaa kufanya vitendo vya kihalifu.
Kamanda Kova amesema katika maeneo ya starehe wananchi wanatakiwa kuwa waangalifu kwa kutokunywa vileo kupita kiasi, kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuzua ugomvi na mambo mengine kama hayo.
Pamoja na mambo mengine, watumiaji wa magari wanakumbushwa kupaki magari yao sehemu zenye usalama na wayafunge vizuri yakiwa na mifumo ya kiusalama (alarm system) ili pindi mhalifu anapotaka kutenda uhalifu aweze kubainika kwa urahisi na haraka.
*DAR ES SALAAM BILA UHALIFU INAWEZEKANA*