Hawa ndio Mabalozi wapya walioteuliwa na Rais Kikwete

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ameteua mabalozi wapya watatu kujaza nafasi zilizoachwa wazi na mabalozi waliostaafu kwa mujibu wa sheria na mwingine kushika Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete


Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule ilisema Rais Kikwete amemteua Dora Msechu kuwa Balozi wa Tanzania Sweden kuchukua nafasi ya Balozi Mohamed Mzale ambaye amestaafu.
Hadi uteuzi huo, Balozi Msechu alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika wizara hiyo.
Pia amemteua Luteni Jenerali Wynjones Kisamba kuwa Balozi wa Tanzania Urusi. Kabla ya uteuzi huo, Jenerali Kisamba anayekwenda kuchukua nafasi ya Balozi Jaka Mwambi, alikuwa Mkuu wa Utendaji Kivita na Mafunzo, Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
Rais pia amemteua Joseph Edward Sokoine kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kabla ya uteuzi huo, Sokoine alikuwa Ofisa Mambo ya Nje Mkuu na Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania, Canada.
Previous Post Next Post