Al Ahly ilivyoizima ndoto ya Yanga

Ndoto za mabingwa wa soka Tanzania bara,Yanga ya Tanzania kutinga hatua ya 16 bora katika michuano ya Soka klabu Bingwa barani Afrika,imefikia ukingoni baada ya kutolewa kwa mikwaju ya penalt 4-3 na Al Ahly ya Misri hapo siku ya jumapili usiku mjini Alexandria.

Katika Mechi hiyo hadi dakika tisini zinamalizika wenyeji Al ahly walikuwa wameshinda bao 1-0, hali iliyolazimu kutumika sheria ya mikwaju ya penalti kufuatia ushindi wa Yanga wa bao 1-0 katika mechi ya awali jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.



Haikuwa siku ya bahati kwa Yanga baada ya awali mlinda mlango wake Deogratias Munisi almaaruf Dida kupangua penalt mbili kati ya tano za awali, ila wapigaji wa upande wa penalti wa upande wa Yanga walishindwa kutumia fursa kujaza mipira nyavuni, ambapo penalti ya mwisho iliyotaraji kuwavusha Yanga ilitolewa nje na mpigaji Said Bahanuzi, na hivyo kukamilisha penalti tano tano,kila timu ikiwa imekosa penalt mbili mbili.

Katika penalt za nyongeza Al Ahly walipata penalty ya sita huku Mbuyu Twite wa Yanga akikosa penalti yake muhimu iliyohitimisha safari ya Yanga kwenye michuano hiyo mwaka huu 2014.

Baada ya kuweka historia kwa upande wake kwa kuifunga Al Ahly bao 1-0 katika mechi ya awali jijini Dar es Salaam, Yanga ilikuwa na matumaini makubwa ya kuandika historia nyingine kwa kuilaza Al Ahly iliyokuwa ikicheza nyumbani.
Previous Post Next Post