Mr.Chuz ataja mambo kumi (10) muhimu yanayomsaidia katika kazi zake na maisha kila siku. Yanakuhusu.

Mtayarishaji wa filamu na Mkurugenzi wa Kundi la Tuesday Entertainment Ltd, Tuesday Kihangala maarufu Mr Chuzi, amezitaja sababu 10 zinazomfanya aendelee kuwepo na kufanya vizuri kwenye tasnia licha ya kuwepo kwa tuhuma nyingi na tofauti dhidi yake. Muigizaji huyo alitaja sababu hizo alipokuwa akizungumza na mwandishi Kalunde Jamal wa mtandao wa mwananchi Mwananchi kama zifuatavyo.


1.Kukubali changamoto zenye msingi
Anasema kuwa yeye kama binaadamu kuna vitu ambavyo hukosea, hivyo anapopata mawazo kutoka kwa watu wengine, yakiwa mazuri au mabaya huyafanyia kazi na anapoona kuna ukweli hujirekebisha au kuboresha palipo na upungufu.
“Hakuna mkamilifu na hakuna ubishi kuwa changamoto ni sehemu ya kujifunza na kujiongezea ujuzi; ndiyo sababu nazikubali kuzifanyia kazi,”anasema Mr Chuz.


2.Kuheshimu jinsia
Anabainisha kuwa hakuna kazi ngumu kama kufanya kazi na watu wa jinsi tofauti (mwanamke na mwanaume), lakini kwa nafasi yake ya ukurugenzi hilo amelipa kipaumbele.
“Namheshimu kila ninayefanya naye kazi, iwe mwanamke au mwanaume mwenzangu. Lakini kama itatokea nikawa na uhusino na mwanamke ninayefanya kazi naye, hayo yatakuwa ni makubaliano ya nje ya kazi, kwani mapenzi ya shuruti katika namna ya utendaji kazi ni sumu ya mafanikio,”anasema Chuz.
3.Kuwa na ushawishi
Anasema kuwa anajitahidi kadiri ya uwezo wake kuwa na ushawishi kwa anaofanya nao kazi, hata wengine ambao wanafanya kazi pamoja ili kuyapa nguvu mawazo yake. “Bila kuwa na ushawishi, wakati mwingine kufanya kazi inakuwa ngumu, unaweza kuwa na wazo lenye msingi wa mafanikio mbele ya safari, lakini kwa kuwa watu hawakuamini yaani hujaweza kuwashawishi wakuamini kama kiongozi, ni ngumu kufikia malengo,”anasema.

4.Kusoma alama za nyakati
Anafafanua kuwa kwa hali ya soko la filamu ilivyo sasa ni lazima kusoma alama za nyakati kwa kuwa unaweza kupoteza nguvu kwa kufanya kitu ambacho hakitaleta mafanikio.
“Natumia muda mwingi kuangalia nifanye nini kulingana na wakati uliopo, badala ya kukurupuka na kufanya ninachokiamini,”anasema na kuongeza:
“Kwa kutambua soko linataka nini, naanzia hapo; lakini vile vile kujua sokoni kuna nini ni silaha kubwa ya mwanzo wa kila safari mpya kwenye kazi yangu.”

5. Kukubali kuwa mwanafunzi siku zote
Anaeleza kuwa tangu alipoanza kazi ya uigizaji, hata utayarishaji  filamu hajawahi kuwa mwalimu, zaidi ya kuwa mwanafunzi.
Anasema kuwa amekuwa akijifunza kutoka kwa wengine, ili kuongeza ujuzi na kujikosoa pale alipokosea.
“Naamini kujua sana ni kasoro walizonazo baadhi ya wanadamu na siku zote zimewafanya wabaki pale walipo. Mimi siyo mmoja wao, najifunza kila siku kutoka kwa wengine ambao hata nikiwataja, hawataamini kuwa najifunza kwao. Hiyo ni sehemu ya silaha zangu za maangamizi ya kuhakikisha nakuwemo kwenye tasnia hii kwa miaka mingi ijayo,”Mr Chuz anaweka wazi.
6.Kuonyesha uwezo binafsi
Kwa nafasi yake ya ukurugenzi, analazimika kuonyesha uwezo binafsi kwa kufanya vitu vya ziada ili kuwapa moyo walio nyuma yake.
“Kama unavyojua, waigizaji siku hizi wapo wengi na wana vipaji, hivyo ni jukumu langu kama kiongozi kufanya kitu tofauti kuanzia kwenye tabia, mavazi, kuamrisha, kukosoa na hata kufundisha kama ikibidi,”anasema.

7. Kusimamia nidhamu kwa kufanya uamuzi sahihi
Anaitaja silaha nyingine kuwa ni kusimamia nidhamu na haki, badala ya kutoa uamuzi wa upendeleo au kumpa haki asiyokuwa nayo kwa maslahi binafsi.
“Nikiwa kazini sina kujuana, nakuwa muwazi ‘black and white’, bila kujali nani atasema nini na wakati gani. Hii ni kwa sababu, kuna kipindi yule unayemtegemea kwenye kazi ndiyo anaongoza kwa nidhamu mbovu; basi ikibidi hasara na iwe hasara, kuliko kuendelea kuwa na mtu wa namna hii. Kwangu hapo kinachofuata ni sheria kuchukua mkondo wake. Sheria kuu ni kuwa na nidhamu, kama huna nidhamu hufai kuwa upande wangu,”anasema Chuz.

8. Kujipanga kwa ujio mpya bila kujali hasara, muda
Anaeleza kuwa ili kutimiza baadhi ya nguzo zake za kazi, inamlazimu kujipanga kwa muda mrefu kabla ya kutoa kazi mpya(filamu), hivyo ukifika wakati huo hajali hasara, wala muda atakaopoteza, ilimradi kazi iwe nzuri.
“Kuna wakati kufanya kitu kizuri kunakatishwa tamaa na maandalizi ya muda mrefu, ikiwemo kurekebisha makosa yanayojirudia, lakini kwa kuwa nimeazimia kufanya kitu tofauti, siku zote huwa silijali hilo, hata kama kazi tutaifanya kwa miezi sita au mwaka, cha msingi iwe bora,”anasema.

9. Maudhui tofauti
Anaeleza kuwa maudhui ya filamu nchini yamekuwa ni tatizo, hivyo ili kufanya kitu kipya ni vyema kwenda mbali zaidi, jambo ambalo wakati mwingine ni vigumu kukubaliwa, hata na waigizaji ambao wamekariri baadhi ya vitu. Lakini kama kiongozi, inakulazimu kuwashawishi watu hadi wakubali na kufanya kitu sahihi na tofauti.
“Maudhui ni silaha kuu kama siyo ngao, hivyo hapa nakuwa makini kupita maelezo na kuleta kitu tofauti, kukwepa kurudia kasoro zilizowahi kufanywa na watu wengine, hiyo imenisaidia na kujenga taswira mpya,”anasema Mr Chuz.


10. Umoja na kuamini ninaofanya nao kazi
Umoja ni silaha ya kuendesha kampuni, hivyo kila ninayefanya kazi naye namwamini na kumwona yupo sahihi, labda kama atafanya kitu tofauti kati ya nilivyovitaja hapo mwanzo, kosa kuu likiwa ni kwenda kinyume na suala la nidhamu.

Previous Post Next Post

Popular Items

WAKUU WA USALAMA KUHOJIWA KENYA