NILISHINDWA KUFUATA MASHARTI YA KUMILIKI BASTOLA NIKAAMUA KUIRUDISHA

Msanii wa kundi la Tip Top Connection Khalid Ramadhan aka Tunda Man, alikuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa wanamiliki silaha za moto (bastola), kitu kilichofahamika na kuandikwa na baadhi ya vyombo vya habari mapema mwaka huu.



Tunda amesema kwa sasa hamiliki tena bastola, sababu aliamua kuisalimisha silaha hiyo aliyokuwa anamiliki kutokana na masharti mengi ya kuimiliki.

“Mimi imenishinda mpaka nimerudisha, Kwasababu watu wengi walikuwa wanajua mimi nilikua na bunduki halafu maneno yakawa mengi”. Alisema Tunda leo katika kipindi cha XXL cha Clouds FM




Tunda amesema kati ya masharti yaliyomshinda ni pamoja na aina ya mavazi anayotakiwa kuyavaa mtu anayeimiliki .

“Kuna mavazi unatakiwa uvae kidogo, mavazi ya kipapaa yale, sometimes unatakiwa uwe nayo muda wote, kuna vitu vingi…watu wasijue kwahiyo watu washajua watu kibao kuwa mimi nina ile, afu kuna watu wanazitafuta zile ili wafanyie mambo yao”. Alimaliza.

Mwezi wa pili mwaka huu gazeti la Ijumaa liliandika habari isemayo ‘SOO LA BASTOLA, TUNDA MAN AKIONA CHA MOTO’.

Hiki ndicho kilichoandikwa katika gazeti hilo:

‘TABIA ya baadhi ya mastaa kuonyeshaonyesha bastola hadharani kimemtokea puani ‘memba’ wa Kundi la Tip Top Connection, Khalid Ramadhani ‘Tunda Man’ baada ya hivi karibuni kuitwa na jeshi la polisi na kuhenyeshwa.

Akizungumza na Ijumaa hivi karibuni Tunda Man alisema makala iliyotoka kwenye gazeti ndugu na hili la Ijumaa Wikienda ikieleza jinsi baadhi ya wasanii wanavyozianika silaha kiholela imemfanya akione cha moto kwani wakati akizungumza na mwandishi wetu alikuwa Kituo cha Polisi cha Kati (Central) akihojiwa.

“Kwanza naomba nikwambie kuwa hakuna kitu ambacho kimenikosesha amani leo (Jumatatu) kama hii habari yako uliyoandika kwenye gazeti, hivi ninavyoongea na wewe niko ‘sentro’ nikihojiwa, kiukweli sina amani,” alisema Tunda Man.

Hivi karibuni msanii wa muziki, Aboubakar Chende ‘Dogo Janja’ alinaswa akiwa na bastola na alipoulizwa ni ya nani alidai ni ya Tunda Man hivyo kumpa msala mwenzake’.



SOURCE: GLOBAL PUBLISHERS 
Previous Post Next Post