Ilikuwa ni saa chache baada ya Rais wa aliyemaliza muda wake wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF), Leodegar Tenga kuwaonya wajumbe wa Mkutano Mkuu kujiepusha na ushawishi wa rushwa katika uchaguzi huo, baadhi ya wagombea waliziba masikio na kujikuta wakiishia kulala lupango.
Taarifa zinasema wajumbe wawili majina tunayo, usiku wa kuamkia jana walilala kwenye Kituo cha Polisi Tabata wakituhumiwa kupokea hongo ya Sh3 milioni sambamba na majina ya wapigakura usiku wa kuamkia jana.
Habari za ndani ambazo gazeti hili ilizipata kutoka ndani ya wagombea hao, zilisema kuwa baada ya watuhumiwa hao kukamatwa waliwataja wagombea waliowatuma kugawa fedha hizo kwa lengo la kuomba kura.
Hata hivyo watuhumiwa hao waliachiwa kwa dhamana jana asubuhi huku kesi hiyo inatarajiwa kuhamishwa kwenye Taasisi ya Kupambana na Rushwa Takukuru leo kwa hatua zaidi.(P.T)
Wakati hayo yakiendelea, katika hali ya kushangaza kwa mara ya kwanza Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF, Hamidu Mbwezeleni alilitaka Jeshi la Polisi kuwazuia wanahabari kushudia uchaguzi huo bila ya kueleza sababu ya kuchukua uamuzi huo.
Ofisa mmoja wa polisi aliyekuwa akisimiamia ulinzi alisema, "Nimesema poteeni kwenye eneo hilo, narudia tena hamtakiwi kuonekana eneo hili poteeni kabla hatujatumia nguvu ya ziada."
Mara baada ya tafrani hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (Taswa) Juma Pinto alisema kuwa leo wanatarajia kuwasilisha barua ya malalamiko kwenye shirikisho hilo.
"Alichokifanya Mbwezeleni ni udhalilishaji wa hali ya juu, aandishi wapo hapa toka saa tatu asubuhi, hajasema chochote, huu utaratibu gani hata kama ni utaratibu mpya alipaswa kutujulisha mapema sio hivi kukurupuka na kuzuia watu."
"Hatuwezi kukubali udhalilishaji huu kwani walitupa semina ya nini, walitenga sehemu ya kukaa waandishi ya nini, kama Taswa kesho (leo) nawasiliana na TFF ama watuombe radhi au la tutatoa tamko lingine zaidi juu ya TFF," alisema Pinto.
Awali mgombea wa nafasi ya ujumbe kupitia kanda namba 12- Kilimanjaro na Tanga, Davis Mosha alilalamikia kitendo cha kamati ya uchaguzi kuwaweka kwa muda mrefu bila ya kujua nini kinaendelea.
"Tupo hapa hatujapewa hata vitambulisho au ratiba ya nini kinaendelea wakati sisi ni wagombea, hatufahamu kuna ajenda gani hapa," alisema Mosha.
Naye Iman Madega alisema tumekaa hapa tangu asubuhi hadi saa hizi ni mchana kinachoendelea hatujui, uko juu.
"Tunashindwa hata kwenda kula kwa sababu hatujui tunatakiwa muda gani, tumelipa fedha angalau tupewe hata maji, wanashindwa basi wangetugaia ratiba," alilalamika Madega mgombea wa nafasi ya makamu wa rais.
Hata hivyo mwisho wagombea wote waliruhusiwa kuingia kwenye ukumbi wa mkutano baada ya malalamiko hayo.
Chanzo:Mwananchi
Tags:
Sports