Mwandishi wa habari wa kutoo cha runinga cha ITV, Ufoo Saro amelazwa kwenye chumba cha wagonjwa wa dharura cha hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam baada ya kupigwa risasi na anayedaiwa kuwa mchumba wake.
Ufoo Saro, kulia akiwa na Rais Jakaya Kikwete
Katika tukio hilo lililotolea leo asubuhi, mama mzazi wa Ufoo ameuawa huku mchumba wake huyo naye akijiua kwa kujipiga risasi.
Taarifa zinadai kuwa mtu huyo ambaye amefahamika kwa jina la Mushi na kwamba alikuwa mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa, alikuwa kwenye mazungumzo ya kawaida na wawili hao huko Kibamba ambapo walishindwa kuelewana na ndipo aliwapiga risasi.
Akiongea na waandishi wa habari leo kwenye hospitali ya Muhimbili, Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi amesema Ufoo anaendelea vizuri na anaweza kuongea kwa sasa na kwamba ana imani atapona na kuendelea na kazi kama kawaida.
Mengi akiongea na waandishi wa habari nje ya kitengo cha dharula hospitali ya Muhimbili. Pembeni ni Afande Ahmed Msangi (Picha: Jamii Forums)
Sababu za tukio hilo bado hazijafahamika lakini kwa mujibu wa chanzo kimoja, linaweza kuwa limetokana na ugomvi wa kimapenzi kati yao.
“Alikuwa mume mtarajiwa wa Ufoo ila jamaa alikuwa akifanya kazi UN nchini Sudan Kusini ingawa kitengo chake bado hakijafahamika ila kwa habari za mtaani zisizokuwa na uhakika wanasema alikuwa mwanajeshi. Anaitwa Mushi. Bwana mushi alikuwa na mgogoro na Ufoo mpenzi wake ila mama mkwe akawa anamtetea Ufoo. Huyu dada alikuwa na mtu wa pembeni ikabuma. NIPO ENEO LA TUKIO,” kimesecha chanzo hicho japo binafsi Bongo5 haijazithibitisha.
Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Hemed Msangi alisema Ufoo alipigwa risasi tumboni na begani na madaktari wanahangaika kuhakikisha wanaokoa maisha yake. Madaktari wameomba apumzike kwa sasa na hivyo hakuna mwandishi aliyeruhusiwa kuingia ndani wala ndugu zaidi ya Mengi peke yake.
Nayo Jamii Forums wameandika:
Inasemekana kulikua kuna ugomvi kati ya wawili hao ambapo walishindwa kuelewana na ndipo walipoamua kwenda kwa mama mzazi wa Ufoo Saro(mama mkwe) ili awasuluhishe.
Baada ya usuluhishi kuanza na kuonekana kuwa tatizo liko kwa mwanaume, mwanaume huyo alimshutumu mama mkwe wake kwamba amekuwa na mazoea ya kumtetea mwanae na ndipo alipotoa bastola na kumpiga mama yake na Ufoo Saro risasi ya kichwa na kumuua papo hapo…. Alipomuua mama huyo, mwanaume huyo alimpiga Ufoo Saro risasi mbili, moja ya tumboni na nyingine ya mguuni na kudhani kwamba amemuua kumbe amemjeruhi tu kisha kujipiga mwenyewe risasi ya kidevuni na kufariki dunia hapo hapo.
Inadaiwa kuwa kufuatia tukio hilo polisi wamegawanyika katika timu tatu ambapo moja ipo Muhimbili, ya pili Kibamba yalipotokea mauaji na ya tatu inashughulika mtaani kutafuta taarifa muhimu za mauaji.
Source: Jamii Forums, ITV, Michuzi, Mchomeblog