Hivi Jinsi Youtube inavyoweza kuwapa wigo wasanii ambao hawajarekodi bado – The Justin Bieber Story




Ukiwa na kipaji cha kuimba, sio lazima uende moja kwa moja studio na kwenda kurekodi wimbo ili upeleke redio. Bahati mbaya ama pengine nzuri, wasanii wengi wa Tanzania na hata nchi nyingi za Afrika huamini hatua ya kwanza ili kuonesha vipaji vyao ni kwa kurekodi wimbo na kuanza kuhangaika kusambaza CD kwenye vituo vya radio.



Na ukweli ni kwamba, hakuna mchakato mgumu kama kusambaza wimbo wako kwenye redio. Kwa mazingira ya Tanzania ambapo uzuri wa wimbo si kigezo cha kupokelewa na kuanza kuchezwa moja kwa moja, nyimbo nyingi huishiwa kapuni ama kutambulishwa mara moja tu na ukasahaulika kabisa.

Ni wachache wenye bahati ya kupeleka wimbo na ukapenya hadi ukawa hit. Hata hao wachache, hupata nafasi hiyo kwasababu mbalimbali zikiwemo kutoa hela ya promo, kutumia watu wanaojuana na watangazaji wengi na wengine ni bahati zao tu.

Lakini kuna namna nzuri zaidi ya wasanii wachanga wa Tanzania wanayoweza kuitumia hata kabla ya kufikiria kwenda kurekodi studio. Na tena hii inawafaa zaidi wale ambao hawana hela ya kulipa studio. Ni ngumu kumsimamisha mtu barabarani na kumwambia ‘Bro mimi nina kipaji cha kuimba naomba unisikilize ninavyoimba’ na akakuelewa.

Lakini.. ukichukua camera ya simu yako, ukajirekodi vizuri ukiimba kwa uwezo wako wote na kwa hisia, tena nyimbo za wasanii wakubwa zilizo maarufu kwa watu, kisha ukiiupload kwenye Youtube, ukashare kwa marafiki zako kwenye mitandao yako ya kijamii, hususan Facebook na Twitter, hakuna wasiwasi, video itasambaa kwa kasi na ikawavutia watu wengi wanaoweza kukusaidia.

Youtube ni mtandao uliobadilisha maisha ya wengi katika nchi za wenzetu, lakini hautumiwi ipasavyo na wasanii wachanga wa Tanzania. Wasanii wengi wa Marekani na kwingineko, wamegundulika kupitia mtandao huo kwa kuupload video wakiimba nyimbo (cover songs) za watu wengine kuonesha uwezo wao.







Mfano mzuri ni Justin Bieber;
“Meneja wangu alinigundua kwenye YouTube,” Justin Bieber aliiambia MTV News, mwaka 2009. “Alinisafirisha kwa ndege hadi Atlanta kwa mara ya kwanza. Nilikuwa naenda kukutana na watu fulani.”
Hata hivyo siku hiyo haikuwezekana kuonana na watu hao lakini siku nyingine ndipo ndoto yake ilianza kutimia baada ya kukutana na mtu muhimu maisha mwake. “Nilimuona Usher kwenye Range Rover, hivyo nikasema, ‘Man, huyo ni Usher.’ So nikamfuata. Hata hivyo siku hiyo, Usher alikataa kumpa nafasi ya kumsikia Justin akiimba.
“Baadaye aliziona video zangu Youtube na akasema, ‘Man, Ningemwacha mtoto huyu aimbe, na akanileta tena Atlanta. Nilimuimbia na kisha wiki moja baadaye nilikuwa na mkutano na Justin Timberlake. Wote wawili walinitaka.”
Lakini hata hivyo, Usher ndiye aliyemchukua na kumtengeneza Justin Bieber huyu wa leo.
Mwingine aliyegundulika Youtube ni Carly Rae Jepsen wa Canada ambaye video yake mwenyewe aliyoiweka YouTube akiimba wimbo, Call Me Maybe ilimshawishi ,Justin Bieber ambaye alimchukua na sasa ni staa kama yeye. 







Wengine ni Alyssa Bernal, aliyemshawishi Pharrell William baada ya kuweka video YouTube na kumsainisha kwenye label ya, Star Trak.




Hiyo ni mifano tu ya wasanii wa Marekani ambao Youtube iliwapa wigo na kuwakutanisha na watu muhimu kwenye muziki na waliobadilisha maisha yao. Bahati mbaya ni kuwa, kwa wasanii wengi Tanzania, Youtube ni mtandao wa kupost tu video za nyimbo zao walizozirekodi. Wengi hawafahamu kuwa, video ya dakika 2 ilivyorekodiwa kwa camera ya kawaida au hata kwa simu, inaweza kubadilisha maisha yao.
Nini cha kufanya?
Kama wewe ni msanii mchanga, una kipaji cha kuimba ama kucheza chombo chochote cha muziki na ungependa watu wakijue kipaji chako, tafuta namna ya kujirekodi au kurekodiwa na mtu ukiimba nyimbo za watu (cover songs) kwa umakini. Fungua akaunti yako mwenyewe ya Youtube (ukiwa na gmail utakuwa nayo moja kwa moja) na anza kuweka video zinazokuonesha ukiimba nyimbo mbalimbali na kuzipost kwenye Youtube. Fanya hivi mara kwa mara na kama utakuwa muimbaji mzuri, utavutia watu wengi wawe mashabiki wako, na kujiweka sokoni tayari.
Maproducer, mameneja na wadau muhimu wa muziki, wengi wana smartphones zinazowawesha kutazama video kutumia simu zao na hivyo ni rahisi kuziona.
Watu watazionaje video zako?
Kwanza ni muhimu kuwa mtumiaji mzuri wa mitandao ya kijamii kama Facebook na Twitter ambako utakuwa unashare video zako huko kila unaporekodi mpya. Unaweza pia kuwatumia watu wenye followers ama marafiki wengi katika mitandao hiyo ili wakusaidie kusambaza link za video zako. Kama ni muimbaji mzuri, na video zako zinavutia kutazamwa, utajipatia umaarufu na kuwa na mashabiki hata kabla ya kurekodi wimbo studio.
Video zipi zinavutia zaidi?
Ukijirekodi ukiimba acapella peke yake, video haiwezi kuwa na mvuto, hivyo tafuta instrumental za nyimbo unazotaka kuimba au tafuta mtu akupigie kinanda au gitaa wakati ukiimba. Kama unaweza kuimba huku ukipiga chombo cha muziki wewe mwenyewe, utakuwa na advantage zaidi.
Fanya hivyo halafu uone.
Previous Post Next Post