Akiongea na Spika wa Bunge la Uswisi, Maya Graf, Spika Anne Makinda amenukuliwa akisema kuwa Wabunge wengi Wastaafu wana hali ngumu kiuchumi pindi wanapomaliza muda wao.
Yumkini Wabunge wetu wastaafu huwa na hali ngumu kiuchumi baada ya kustaafu, lakini, tafsiri zaweza kuwa nyingi. Si kwamba Waheshimiwa hao hawakuwa wabunifu walipokuwa Mjengoni. Yawezekana baadhi yao wanahangaika sasa kwa vile walikuwa waadilifu sana. Hawakuiba senti za Wananchi.
Kwamba wameitumikia nchi bila kufanya ujanjaujanja na hivyo mitaani kuonekana wako hoi. Maana, kwa mshahara wa kawaida wa Mbunge, kwa kweli kuwa na magari na nyumba za kifahari ni jambo gumu.
Tukumbuke Wabunge hao wana familia zao za watoto wa kuwasomesha , wana pia ndugu na jamaa wanaowategemea. Achilia mbali wananchi wa majimbo yao wenye kuwataka misaada kila kukicha.
Hapa Mbunge mwadilifu kwa kiwango kikubwa hawezi kumaliza kipindi chake akiwa tajiri.
Haya, kwa masengenyo haya, Spika Makinda hatawaona tena Wabunge wenzake Wastaafu wakifika kwa wingi ofisini kwake. Maana, hata wale waliokuwa wakitaka kupita tu kumsabahi Spika, na hata kumpa ushauri wa hapa na pale, nao huenda wataogopa kuonekana ni 'omba omba'.
Na kwa Wabunge hao wastaafu nitawakumbusha wimbo wa kwenye Lizombe, ngoma ya Wangoni, na wanaweza kuingiza maneno yao wakipenda, usikike hivi; ...
" Tulipokuwa Mjengoni wee, Spika hakutusemaa..
Tumeondoka kidogooo, nyuma anatusengenyaa... Weee!"
Naam, dhiki haina mwenyewe!
Maggid.
Tags:
Social