Marekani imesema Jumapili(08.09.2013) haifuti uwezekano wa kurudi tena kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutafuta azimio juu ya mzozo wa Syria mara baada ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kukamilisha repoti yao.
Marekani imesema Jumapili(08.09.2013) haifuti uwezekano wa kurudi tena kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutafuta azimio juu ya mzozo wa Syria mara baada ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kukamilisha repoti yao juu ya shambulio la silaha za sumu na kudokeza kwamba nchi za Kiarabu zinataka nchi hiyo ichukuliwe hatua kali.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Paris baada ya kukutana na mawaziri muhimu wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu, waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema nchi hizo zimekuwa zikielekea kuiunga mkono taarifa ya pamoja ya nchi za kundi la G20 zenye maendeleo ya uchumi duniani ambayo tayari imesainiwa na mataifa 12 inayotowa wito wa kuchukuliwa kwa hatua kali ya kimataifa kufuatia shambulio la silaha za sumu la Augusti 21 nchini Syria.
Serikali ya Marekani na Ufaransa zinasema vikosi tiifu kwa Rais Bashar al-Assad vimehusika na shambulio hilo ambapo zaidi ya watu 1,400 inakadiriwa kuwa wameuwawa na kwamba lazima kiongozi huyo azuiliwe kutumia tena silaha za aina hiyo.
Hollande yuko chini ya shinikizo
Rais Francois Hollande wa Ufaransa ambaye yuko chini ya shinikizo nchini mwake na kutoka washirika wenzake wa Ulaya kutaka ruhusa ya Umoja wa Mataifa kabla ya kuchukuwa hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Syria hapo Jumamosi amedokeza kwamba yumkini akawasilisha azmio kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa licha ya huko nyuma kukwamishwa na kura za turufu za Urusi na China.
Maafisa wa Ufaransa wamesema rasimu ya azmio lililowasilishwa kwa pamoja na Ufaransa na Uingereza mwishoni mwa mwezi wa Augusti hata halikusomwa na Urusi na China ukiachilia mbali kulijadili.
Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa huenda wakakabidhi repoti yao baadae wiki hii pengine katika wakati huo huo bunge la Marekani likipiga kura kuruhusu mashambulizi ya kiwango fulani kwa Syria.
Bado hakuna uamuzi
Kerry amesema "Kuhusu kauli ya Rais Hollande kuhusiana na Umoja wa Mataifa,rais(Obama) na sisi sote tunawasikiliza kwa makini marafiki zetu wote."
"Hakuna uamuzi uliofikiwa na rais".
Baada ya mkutano na waandishi wa habari afisa mmoja wa Marekani amesema nchi hiyo kwa sasa haipiganii kuwasilisha azimio ili kupigiwa kura na Umoja wa Mataifa. Afisa huyo aliekataa kutajwa jina lake amesema daima wamekuwa wakiunga mkono kufanya maamuzi kupitia Umoja wa Mataifa lakini imedhihirika kwamba hakuna njia ya kupiga hatua huko na kwa hivyo kwa sasa hawafikirii kupendekeza kura nyengine katika baraza hilo.
Mkutano wa Kerry na mawaziri wa Kiarabu unazijumuisha Saudi Arabia,Misri,Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu baada ya mazungumzo huko Lithuania na mawaziri wa mambo ya nje wa Ulaya ambao wamemtwika lawama Assad kwa shambulio la sumu nchini Syria lakini wamekataa kuidhinisha hatua ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo.
Kerry akiwa pembezoni mwa waziri mwenzake wa Qatar Khaled al -Atiya amesema "Sote tunakubaliana mashambulizi ya kulaaniwa ya matumizi ya silaha za sumu ya Assad yamevuka mstari mwekundu wa kimataifa."
Kerry hapo Jumamosi(07.09.2013) alikutana na waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius wakati washirika hao wawili wakiwa mbioni kuupanuwa muungano wao wa kimataifa dhidi ya Assad na kubadili maoni ya umma wao.
Fabius amekiambia kituo cha televisheni cha France 3 TV kwamba iwapo hawachukuwi hatua inamaanisha leo au kesho wanatuma ujumbe wa maandishi kwa Assad,kwa Wairani,kwa Wakorea Kaskazini na makundi yote ya kigaidi kwa kuanzia na Al Qaeda kuwaambia endeleeni kutumia silaha za sumu.
Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters
Tags:
Social